Makala

Joho kuongoza mkutano na Rais kujadili mbinu za kufufua uchumi wa Pwani

August 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

UHUSIANO wa karibu kati ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho na Rais Uhuru Kenyatta utamwezesha kupanga mkutano kati ya Rais na viongozi wa Pwani kwa ajili ya kujadili uchumi wa eneo hilo.

Duru ziliambia Taifa Leo kuwa mkutano huo ambao utashirikisha magavana sita, wabunge na madiwani utajadili njia mbadala za kupiga jeki uchumi wa pwani badala ya kutegemea bandari ya Mombasa.

Bandari hiyo imekuwa kitega uchumi kikuu katika eneo hilo kwa miongo kadha.

Ajenda ya kwanza katika mkutano huo wa viongozi, ambao unasemekana utafanyika baada ya kipindi cha wiki moja, itakuwa ni jinsi ya kufaidi kutokana na rasilimali za mafuta na gesi katika eneo la Pwani na mradi wa eneo la kiuchumi la Dongo Kundu.

Rais Kenyatta na Joho wanasema miradi kama hii inaweza kuajiri watu wengi kuliko bandari ya Mombasa.

Wataalam wa masuala ya kiuchumi wameashiri kuwa hali itakuwa ngumu katika eneo la Pwani kufuatia mpango wa serikali kuamuru kwamba mizigo yote kutoka Bandari ya Mombasa yatasafirishwa kwa reli ya kisasa (SGR) na kukaguliwa katika eneo la kuhifadhi konteina (ICD) jijini Nairobi.

Mnamo Jumatano, Gavana Joho alisema wakati umetimia kwa viongozi wa eneo la Pwani kuanza kutafakari kuhusu njia za kupanua shughuli zake za kiuchumi, wazo ambalo linalandana na yake Rais Kenyatta.

“Katika taalam ya uchumi, tunaamini kuwa mtu anafaa kusaka njia za kumwezesha kupanua shughuli za kujipatia mapato kila mara. Hatuwezi kusalia kama zamani,” Joho akasema.

Alisema hayo katika bandari ya Mombasa wakati wa sherehe ya kihistoria ambapo Rais Kenyatta alizindua usafirishaji wa mafuta ghafi, yaliyochimbwa kutoka kaunti ya Turkana, hadi taifa la Malaysia. Sherehe hiyo la mapipa 200,000 italetea taifa hili Sh1.2 bilioni.

“Tunapaswa kujishughulisha na shughuli nyingi za kiuchumi. Hatuwezi kutegemea bandari pekee,” Raia Kenyatta akasema.

Joho alisema viongozi wa Pwani wamegundua kuwa vita vya kisiasa kila mara na serikali havisaidii.

Ngome ya upinzani

Eneo hilo limesalia kuwa ngome ya upinzani kwa miongoni kadhaa zilizopita hali ambayo, wataalamu wanasema, imedumaza maendeleo eneo hilo licha ya kukirimiwa na utajiri mkubwa wa mali asili.

Bw Joho anatumia mazingira mazuri yaliyoletwa na muafaka (handisheki) kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuishawishi serikali kuwekeza rasilimali nyingi katika eneo la Pwani.

“Rais ni kiongozi ambaye anaweza kufikiwa kwa urahisi. Basi hatuna budi kumfikia sisi kama viongozi,” gavana Joho akasema.

Gavana Joho na Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi walisema katika mkutano huo watajadili kero la kupotea kwa nafasi za ajira kufuatia agizo la serikali kwamba mizigo yote ya kwenda maeneo mengine isipokuwa Mombasa ikaguliwe (cleared) jijini Nairobi.

Kulingana Bw Joho, kwa kuwa mafuta yamevumbuliwa katika kaunti ya Turkana, kaunti ya Mombasa inaweza kuanzisha eneo la kibiashara na viwanda vya kuongeza thamani kwa mafuta hayo.

“Tuna uwezo wa kufanya hivyo,’ akasema.

Baada ya kuzindua meli hiyo ya kusafirisha mafuta, kwa jina Celsius Riga, Rais Kenyatta alisafiri hadi Japan kuhudhuria Kongomano la Kimataifa la Tokyo kuhusu Maendeleo Barani Afrika (TICDA).

Alisema mipango ya ujenzi wa eneo la kiuchumi la Dongo Kundu ni mojawapo ya masuala ambayo atajadili pamoja na viongozi wa Japan ili kuvutia wawekezaji katika mradi huo.

Majuma matatu yaliyopita Waziri wa Biashara Peter Munya alichapisha rasmi kwenye gazeti la serikali maeneo ya Dongo Kundu, Naivasha, Konza City na Kisumu katika maeneo maalum ya kiuchumi.

Eneo la Dongo Kundu ni la ukubwa wa ekari 3,000 na kuanzishwa kwa shughuli za kiuchumi hapo kutavutia wawekezaji wa humu nchini na kutoka mataifa ya nje ambao watafurahia vivutio vya kuanzisha viwanda.

“Ukirejea hapa wakati wa kufunguliwa rasmi wa Maonyesho ya Kilimo, tupe nafasi ya saa mbili tukuelezee jinsi ambavyo tungependa kupanua uchumi wetu, kwa nini ni muhimu kwa Mombasa kufikia lengo la kuwa eneo huru la kibiashara na kwa nini ni muhimu kuharakisha mpango wa kuanzishwa kwa mradi wa Dongo Kundu,” Joho akasema.

Gavana huyo pia alisema mradi wa Dongo Kundu utabuni nafasi ya ajira mara 10 kuliko bandari ya Mombasa.

Wakati huu bandari hiyo inaajiri watu 7,000 moja kwa moja.

Munya alisema Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ndilo litaongoza shughuli za ustawishaji wa mradi wa Dongo Kundu.

Mnamo Julai Rais Kenyatta alizindua Taasisi ya Bandari kuhusu Mafunzo ya Ubaharia (Bandari Maritime Academy) na kushuhudia kutiwa saini kwa mkataba kati ya Wizara ya Uchukuzi na Kampuni ya Huduma za Meli ya Meditereanea Shipping Company(MSC).

Mkataba huo ulifufua Shirika la Kitaifa la Huduma za Meli (National Shipping Line).

Kampuni ya MSC kufikia sasa imeajii Wakenya 256 kama mabaharia tangu kutiwa saini kwa mkataba huo.

Kampuni hiyo ya huduma za meli nayo itaajiri jumla ya Wakenya 2,000 kila mwaka.