Makala

MAKALA MAALUM KUHUSU MIHADARATI: Mshukiwa na washirika wake wanavyozidi kukwepa adhabu

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MOHAMED AHMED

POLISI wanajikuna kichwa kutegua kitendawili cha mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati mwenye ushawishi ambaye amekuwa akitumia ujanja kuondoka jela.

Polisi wamekuwa wakimkamata Swaleh Yusuf Ahmed almaarufu ‘Candy Rain’ au ‘Kandereni’ na washirika wake mara kadhaa lakini kila mara amekuwa akiondoka gerezani katika hali tatanishi.

Alianza kama dereva wa matatu mjini Mombasa na muuzaji mihadarati wa kiwango cha chini hadi kuwa mlanguzi maarufu na mwenye ushawishi mkubwa.

Alianza kwa kuuza tembe ziitwazo “bugizi” ambazo hununuliwa sana na watumizi wa kiwango cha chini.

Alikuza biashara yake kwa kutumia uhusiano wake wa karibu na wanasiasa maarufu katika eneo la Pwani, ambao walimpa ulinzi wa kisiasa, hali iliyomwezesha kuipanua sana.

Kadri biashara yake ilivyopanuka, japo si kwa kiwango cha familia ya Akasha, alijipata pabaya, hali iliyosababisha yeye kukamatwa mara kadhaa na polisi.

Baadaye, alikamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani.

Hata hivyo, aliwasilisha rufaa dhidi ya hukumu hiyo, ambapo alifanikiwa kuachiliwa, japo katika hali tatanishi.

Kukamatwa na kuachiliwa kwake kila mara kulionekana kumpa nguvu na ushawishi mkubwa. Familia yake pia ilichangia sana katika upanuzi wa biashara hiyo.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa sawa na ilivyokuwa familia ya Akasha, anawashirikisha mkewe, mpenziwe na shemeji zake kadhaa ambao ni nguzo kuu ya biashara hiyo.

Polisi wanasema kuwa anaonekana kujaza pengo lililoachwa na familia ya Akasha katika biashara ya mihadarati.

Rekodi pia zinaonyesha kuwa biashara yake huwa inapata faida sana kutokana na ushawishi mkubwa alio nao miongoni mwa maafisa wa idara za usalama na sheria.

Miongoni mwa washirika wake wakuu ni Bw Mwasuo Bakari Tajiri, ambaye amemuoa shemeji yake.

Bw Tajiri amekamatwa mara tatu akiwa na dawa aina ya heroin zenye thamani ya mamilioni ya pesa, lakini amekuwa akifanikiwa kuachiliwa hata baada ya kufikishwa mahakamani.

Kwa sasa, Bw Tajiri anakabiliwa na kesi tatu za ulanguzi wa mihadarati katika mahakama moja ya Mombasa, lakini ameachiliwa kwa dhamana katika kesi hizo zote.

Alikamatwa mnamo mwezi Juni akiwa na kilo 1.4 za heroin zenye thamani ya Sh3.1 milioni.

Mnamo Aprili, mshukiwa, ambaye ni raia wa Tanzania, alikamatwa pamoja na mwanamke mwingine aliyetambuliwa kama Fatuma Mohammed Sikobo, akiwa na kilo tatu za heroini zenye thamani ya Sh3 milioni katika eneo la Nyali, jijini Mombasa.

Mnamo 2017, alikamatwa tena kwenye msako uliowalenga raia wa Italia waliotuhumiwa kushiriki katika biashara hiyo, ambapo alipatikana akiwa dawa aina ya heroin zenye gharama ya Sh10 milioni, pesa na silaha.

Rekodi za polisi zinaonyesha kwamba awali, Tajiri alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kutokana na wizi wa kimabavu, lakini akaachiliwa mnamo 2015 kufuatia msamaha wa rais.

Walanguzi hao wawili wana uhusiano wa karibu, kwani wamewaoa dada wawili; Asman Abdallah, mkewe Kandereni na Halima Abdallah, ambaye ni mkewe Tajiri.

Dada hao wawili wanatoka katika eneo la Kisauni, Mombasa. Asman alikamatwa na polisi pamoja na mumewe mnamo 2017 ambapo walipatikana na kilo 17 heroin zenye thamani ya Sh170 milioni na Sh18.5 milioni pesa taslimu.

Vilevile, polisi walitwaa magari kadhaa ya kifahari ya Kandereni ambayo yanaozea katika makao makuu ya polisi, Mombasa.

Dada aangaziwa

Si mengi yamesikika kuhusu Asmah tangu kukamatwa kwake na polisi, kwani wamekuwa wakimwangazia pakubwa dadake, Halima.

Jina lake lilikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa zaidi na polisi katika eneo la Pwani kwa kujihusisha na biashara ya mihadarati.

Dawa zenye thamani ya Sh18 milioni zilipatikana kwenye msako uliofanywa juzi na polisi.

“Halima Abdallah Mohamed, mkewe Masuo Bakari Tajiri anaaminika kuwa mshirika wa karibu wa mtandao wa dawa za kulevya unaoongozwa na Swaleh Ahmed au “Candy Rain” anayekabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa zaidi ya kilo 100 za heroin,” inaeleza ripoti ya polisi.

Dawa hizo, zenye thamani ya Sh300 milioni zilinaswa katika nyumba moja na polisi katika eneo la Kikambala, Kaunti ya Kilifi mnamo Septemba 20 mwaka uliopita.

Kunaswa kwa dawa hizo ndiko kuliwafanya polisi kuanzisha msako mkali dhidi ya Bi Fatuma Ali Ahmed, ambaye ni mpenzi wa Kandereni aliyekamatwa katika mtaa wa Eastleigh, jijini Nairobi mwaka 2018.

Polisi walisema kuwa Fatma ndiye alikuwa msimamizi wa makazi ambapo dawa hizo zilinaswa.

Wakati wa kukamatwa kwake, Fatma alikuwa akiendesha duka la M-Pesa jijini Mombasa.

Mshirika mwingine wa mtandao huo ni Zainab Abdi Farah, ambaye polisi walisema kwamba huwa anasambaza dawa hizo katika eneo la Kisauni.

Bi Farah, ambaye alikamatwa mara ya pili wiki iliyopita, ni mwanawe Bi Salma Bakari, 62. Wawili hao walikamatwa mnamo mwezi Mei wakiwa na dawa aina ya heroin, zenye thamani ya Sh3 milioni.