• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
‘Jinamizi la ajali nchini linahitaji kutathminiwa kwa kina’

‘Jinamizi la ajali nchini linahitaji kutathminiwa kwa kina’

Na SAMMY WAWERU

SAFARI ya mwanamuziki tajika wa benga kwa lugha ya Agikuyu, John Ng’ang’a Mwangi maarufu kama John De’ Mathew, duniani ilifikia kikomo mnamo Jumapili usiku Agosti 18, 2019.

De’ Mathew aliripotiwa kuaga dunia baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabara eneo la Blue Post Hotel, Thika.

Kwenye hafla yake ya mazishi eneo la Gatanga kaunti ya Murang’a mnamo Agosti 24 viongozi wakuu serikalini akiwamo Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake Dkt William Ruto, mawaziri kadhaa, viongozi wa kisiasa na wanamuziki walihudhuria miongoni mwa waombolezaji wengine.

Mwendazake alimiminiwa sifa chungu nzima na kila aliyepata fursa ya kumuomboleza jukwaani. Rais Kenyatta alimtaja kama muimbaji anayepaswa kuigwa kutokana na ukarimu wake na ukwasi wa moyo kusaidia.

“Historia ya maisha ya John De’ Mathew ni ya kutia motisha. Alitumia kipaji chake kuboresha maisha ya wasiojiweza,” akasimulia Rais, akieleza kuhusu ukuruba kati yake na De’ Mathew hasa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017.

Hata ingawa baadhi ya vibao vyake vilikosolewa na kukashifiwa kucharura wapinzani wa chama tawala cha Jubilee, umaarufu wake hasa eneo la Mlima Kenya aliutumia kufanyia Rais Kenyatta na Naibu wake kampeni.

Huzuni ilitanda wanawe wakisoma risala kumuaga baba yao, na kila mwombolezaji aliyehudhuria hafla hiyo pamoja na walioifuatilia kupitia runinga zilizopeperusha moja kwa moja wakilengwa na hata kutiririkwa na michirizi ya machozi.

Mmoja wa binti zake, alifichua kwamba kwenye jinamizi, kabla ya kifo chake alionyeshwa babake amehusika katika ajali.

“Nilipopokea habari za huzuni kuhusu maafa ya baba, nilivuta mawazo nyuma ndoto niliyoota. Ni pigo ambalo kufikia sasa limeacha pengo kubwa. Siamini sitakuwa nikipiga pasi nguo za baba,” alisema mtoto wake wa kike.

Licha ya majinamizi ya ajali nchini kuwa kero kuu, viongozi waliohutubu katika mazishi ya Demathew hususan kutoka serikalini hakuna hata mmoja aliyegusia suala hilo. Wote walionekana kuegemea masuala ya siasa, Rais akikashifu wanaosakata siasa za urithi wa Ikulu 2022.

Kwa mtazamo, jukwaa la buriani kwa Bw De mathew lilipaswa kutumika kuhamasisha mikakati kuangazia visa vya ajali. Ni jinamizi ambalo limenyang’anya taifa hili wananchi wengi hasa kwa sababu ya utepetevu miongoni mwa madereva.

Serikali na wadau husika katika sekta ya uchukuzi na usafiri wananyooshewa kidole cha lawama kuchukua hatua hasara inapotokea. Ukifuatilia matukio ya ajali nchini, viongozi hujitokeza na kutoa mapendekezo wakati wa ajali, waliofariki wakizikwa mikakati iliyowekwa inazikwa katika kaburi la sahau.

Sheria za Michuki, zilizoasisiwa na aliyekuwa waziri wa uchukuzi na usalama wa ndani na mikakati ya serikali kuu marehemu John Michuki zinaonekana kupuuzwa.

Hata ingawa mwaka 2018 Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitangaza kufufua sheria hizo za trafiki, kampeni hiyo baadaye ilififia.

Sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya ambazo zisipokodolewa macho ina utepetevu wa hali ya juu. Hii ina maana kuwa sheria za trafiki zisipotiliwa mkazo, maafa yataendelea kushuhudiwa.

Joseph Kago, dereva, anasema usalama barabarani unapaswa kuanzia kwa madereva na wahudumu wa matatu.

“Visa vya ajali vinavyoshuhudiwa nyingi yavyo husababishwa na utepetevu na ukiujaji wa sheria za trafiki. Ni jukumu la kila dereva kuzitii. Wasafiri nao wasikubali kuabiri matatu zinazokiuka sheria,” asema Bw Kago, akihimiza serikali kuongoza katika hamasisho hilo.

You can share this post!

Asimulia jinsi alivyozindua mochari za Montezuma Monalisa

Karani wa sensa aliyechafua makazi ya mtu atozwa faini

adminleo