• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Aliyemfanya mume mtumwa ajuta

Aliyemfanya mume mtumwa ajuta

Na MWANDISHI WETU

ZIMMERMAN, NAIROBI

WANAWAKE wanaoishi kwenye ploti moja mtaani humu walimfokea mwenzao kwa kile walichodai kuwa na tabia ya kumdhalilisha mumewe.

Inasemekana wanawake hao walitishia kumtimua kipusa iwapo angeendelea kumdhalilisha mume wake.

Mdokezi anasema kuwa wapangaji kwenye ploti hawakufurahishwa na namna kipusa huyo alivyokuwa akimchukulia bwana yake.

Wengi walidai kwamba alikuwa amemfanya jamaa kuwa mtumwa wake. Mambo yalimuendea mrama wapangaji walipomkuta jamaa akifua nguo huku mwanadada akisimama.

“Wewe ni mwanamke sampuli gani. Mzee wako anawezaje kufua nguo na wewe umesimama. Ifikapo jioni ni yeye yuko jikoni,” wapangaji walimfokea kipusa.

Inadaiwa kwamba mwanadada huyo alijitia hamnazo.

“Huyu ni mzee wangu. Achaneni na nyumba yangu kabisa,” aliwafokea.

Maneno ya kipusa yalikuwa kama chumvi kwenye kidonda.

“Mjinga ndiye wewe. ‘Unatuangusha’ kama wanawake. Acha bwanako pia aishi kama wanaume wenzake. Acha utumwa,” wanawake walimkaripia.

Duru zinasema kutokana na aibu, jamaa aliondoka hapo na kuingia katika nyumba.

“Mzee mzima unampa kazi ya kukuoshea chupi na sidiria. Vyombo ni yeye anaosha. Kwani kazi yako kwa nyumba ni ipi. Bure kabisa,” mwanamke mmoja alisikika akifoka.

Duru zinasema ilimbidi mrembo kunyamaza.

“Nyinyi wasichana wa siku hizi mna shida nyingi sana. Ndiyo maana wanaume wengi wanakataa kuwaoa,” mama mwingine alisikika akisema.

Vicheko vilishamiri ploti nzima. Wengi walishabikia tukio hilo.

“Wewe ni msichana mdogo sana lakini ukiendelea hivi, utamfanya huyu jamaa akutoroke. Yeye si punda wako,” kipusa huyo alikemewa.

Alipoona matusi yamezidi, mwanadada huyo aliamua kuingia chumbani na kujifungia ndani.

“Hata ukijifungia ndani ya nyumba, utatoka tu nje. Kuwa mwanamke anayemjali bwana,” kipusa alifokewa.

You can share this post!

Kenya itaanza kuonja faida ya mafuta baada ya miaka minane

Wakenya wanyakua dhahabu mbili kipute cha Dunia Korea Kusini

adminleo