Wakenya wanyakua dhahabu mbili kipute cha Dunia Korea Kusini
Na ABDULRAHMAN SHERIFF, akiwa Korea Kusini
KENYA ilifanikiwa kupata medali mbili za dhahabu na tatu za shaba kwenye siku ya kwanza ya Mashindano ya 2019 World Martial Arts Mastership Championship yanayofanyika katika ukumbi wa Korea National University of Transport mjini Chungju nchini Korea Kusini.
Timu hiyo ya Kenya inayojulikana kwa jina lake maarufu Jasiri, ilinyakua medali yake ya kwanza ya dhahabu kwenye kitengo cha Sparring kwa wanaume wa zaidi ya uzani wa kilo 90 ambapo Gordon Ochieng alifanikiwa kumshinda Ki Hoon wa Korea kwa 3-2.
Lona Apiyo Abiero akashindia Kenya dhahabu ya pili kwenye kitengo cha Sparring kwa wanawake wa uzani chini ya kilo 65 baada ya kumyuka Nattakarn Khamsopmpond wa Thailand kwa 5-4.
Peter James Njuguna aliipatia Kenya medali ya shaba kwenye kitengo cha Sparring kwa wanaume wa uzani chini ya kilo 90 aliposhindwa na Mohammadreza Dolatiyan kwa 7-3 kwenye pigano la robo fainali.
Dolatiyan ndiye aliyeshinda medali ya dhahabu.
Mshindi mwingine wa medali nyingine ya shaba alikuwa Patricia Lucky kwenye kitengo cha Sparring kwa wanawake wa uzani chini ya kilo 50 ambaye alishindwa na Unjung Ai Moonville Estarabela wa Phillipines kwa 8-0.
Salma Ali Abdalla pia aliipatia Kenya medali ya shaba baada ya kushindwa kwenye nusu fainali ya Individual Form kwa wanawake.
Ochieng alisema alifanya mazoezi magumu kwa ajili ya mashindano hayo na ziara yao ya kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ilimpa motisha ya kutaka kupigania medali ya dhahabu.
“Nililala kuchelewa Jumatano usiku na nikaamka mapema alfajiri ya Alhamisi nikifikiria vipi nitapigana kuwapa Wakenya wenzangu huko nyumbani kuwashindia medali ya dhahabu,” akasema.