MBURU: Raia wahamasishwe kuhusu athari za uchafuzi wa mito
Na PETER MBURU
SERIKALI imeendelea wiki hii na kampeni ya kuadhibu kampuni zinazolaumiwa kwa uchafuzi wa chemichemi za maji katika sehemu tofauti za nchi.
Hatua hiyo inafuatia habari zilizochapishwa hivi majuzi kuhusu jinsi mito ya Nairobi imegeuzwa jaa la taka na kinyesi na hivyo kuhatarisha maisha ya wenyeji.
Katika msururu wa hatua hizo, baadhi ya viwanda vimefungwa na vingine kuonywa na kushauriwa kuchukua hatua mwafaka za kurekebisha hali hiyo. Huku hayo yakiendelea, baadhi ya taasisi za serikali zinazosimamia usafi wa mazingira zimejitahidi kuonyesha makali yao kwa kuadhibu vikali kampuni zinazolaumiwa kuchafua mito, kwa kumwaga uchafu wenye kemikali.
Viwanda husika vimelaumiwa kuwa vimekuwa vikichafua maji yanayotumiwa na watu nyumbani na pia wakulima, hali ambayo inasababisha hatari za kiafya kwa maelfu ya Wakenya ambao hutumia maji hayo.
Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa katika hatua hii ya serikali kuanza kuharakisha kurekebisha hali hii. Kwanza, mashirika husika ya serikali yanaonekana kama kwamba hayajakuwa yakifanya kazi zao ipasavyo, kwa kuwa yameanza kujitokeza baada ya vyombo vya habari kufichua kuhusu hali ya hatari inayokumba maelfu ya Wakenya.
Hali hii ni ishara wazi kuwa mashirika haya, ambayo yamepewa majukumu ya kuhakikishia Wakenya usalama wa kiafya kutokana na maji wanayotumia, hayana uwezo wa kufanya kazi bila kumulikwa. Ni hali ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika idara nyingi za serikali na ambayo sasa sharti ikomeshwe.
Pili, wananchi ambao wanaishi karibu na mito sasa wanafaa kufahamu kuwa kutupa takataka katika chemichemi hizo za maji ni hatua isiyofaa si tu katika kampeni za kudumisha usafi wa mazingira, bali usalama wa maisha yao. Kinaya ni kuwa wote; wanaochafua na wasiochafua wanaishia kuwa waathiriwa wa uchafuzi wa maji na mazingira, kwani magonjwa yanapoanza kusambaa hayabagui yeyote.
Ni vyema wakazi walio karibu na mto, wasimamizi wa viwanda na mashirika ya serikali yaliyojukumiwa kuhakikisha maji ni salama kwa matumizi ya binadamu, kufanya kazi zao kwa makini ili kuhakikisha kuwa maji hayachafuliwi, ili kuepusha raia kutokana na maambukizi ya maradhi kama kansa. Vilevile, ni vyema watumiaji wawe wakiyachemsha kabla ya kunywa ili kuepuka maradhi.
Vile vile, ni matumaini ya Wakenya wengi kuwa kila mshikadau katika jamii atajitolea kulinda mazingira na chemichemi za maji kwa kuwa huo ndio uhai wa kila mmoja. Mashirika kama NEMA pia yafanye uhamasisho wa kitaifa kuhusu usafi wa mazingira.