• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 3:55 PM
Kibwana akana madai ya kufanyia kazi Tangatanga

Kibwana akana madai ya kufanyia kazi Tangatanga

Na PIUS MAUNDU

GAVANA wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya wandani wa kinara wa chama cha, Bw Wiper Kalonzo Musyoka kuwa amejiunga na mrengo wa TangaTanga unaompigia debe Naibu Rais, Dkt Rais William Ruto.

Prof Kibwana ambaye amejiunga na orodha ya wanaowania Urais mwaka wa 2022, amesema madai kwamba amejiunga na kambi ya Dkt Ruto yanaenezwa na watu wanaohofia umaarufu wake eneo la Ukambani.

Madai hayo yalienea majuma mawili yaliyopita baada ya Prof Kibwana kuandamana na Naibu Rais kwenye ziara ya kiserikali katika kaunti ya Turkana.

Prof Kibwana ambaye anahudumu kipindi chake cha pili, aliwaacha viongozi wengine vinywa wazi, aliposema uwaniaji wa Dkt Ruto haufai kupuuzwa na pia kumrai kumaliza uhasama kati yake na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Ni kutokana na matamshi hayo ambapo wandani wa Bw Musyoka, walimchemkia gavana huyo huku kinara wao pia akikabiliwa na ushindani kutoka kwa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua ambaye pia ametangaza kuwa atakuwa debeni 2022.

Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo, Jumamosi aliambia mkutano wa kisiasa katika Shule ya Upili ya Mathemba kwenye eneobunge lake kwamba Prof Kibwana ni ajenti wa Dkt Ruto eneo la Ukambani.

“Gavana amejiunga na mrengo wa Tangatanga akiwa na nia ya kumdunisha Bw Musyoka. Hatutamruhusu mtu yeyote hapa Ukambani kuwania Urais dhidi ya Bw Musyoka,” akasema, akiunga kauli ya aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama na Seneta wa Kitui Enock Wambua.

Viongozi hao wanaamini kwamba Bw Mutua na Prof Kibwana watagawanya kura chache za jamii ya Wakamba na kuhatarisha azma ya Bw Musyoka ya kuingia ikulu 2022.

Hata hivyo, Prof Kibwana amekanusha kwamba yupo Tangatanga, akisema havumishi uwaniaji wa Dkt Ruto.

“Chama cha Wiper hakitakuwa maarufu kwa kueneza propaganda,” akaeleza Taifa Leo jana.

Gavana huyo ambaye amejizolea sifa kwa kuendeleza ugatuzi kwa njia ya kustaajabisha eneo la Makueni, alivuliwa uenyekiti wa chama cha Wiper kutokana na msimamo wake.

Baraza Kuu la chama hicho majuzi liliidhinisha aliyekuwa mbunge wa Matuga, Chirau Ali Mwakwere awe mwenyekiti wake mpya.

Matamshi hayo makali ya kisiasa yanajiri baada ya Prof Kibwana kukutana na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, akimwomba amlinde dhidi ya shutuma kali ya wandani wa Bw Musyoka.

“Unafaa kutufundisha mtindo wa kisiasa ambao unaendelezwa Magharibi mwa Kenya ili mimi, Bw Musyoka na Dkt Mutua wakieleza nia ya kuingia ikulu, basi hakuna atakayeonekana kuwa msaliti mwenye nia ya kumharibia mwenzake,” akasema Prof Kivutha.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi aliwaomba wandani wa Bw Musyoka kuruhusu demokrasia itambe ukambani na kukoma kuwadunisha wanaopinga azma ya makamu huyo wa zamani wa Rais.

Bw Mudavadi ambaye pia ametangaza azma ya kuwania Urais 2022, alisema kwamba hakuna tatizo lolote iwapo magavana hao wawili wangependa kutoa upinzani kwa Bw Musyoka.

“Hakufai kuwe na uhasama wowote iwapo wanasiasa kutoka eneo moja wangependa kuwania Urais 2022,” akasema Bw Mudavadi mjini Wote baada ya kuandaa mazungumzo ya kina na Prof Kibwana katika afisi za kaunti.

You can share this post!

Kenya Power kutumia Sh9.5b kuunganisha umeme Nyanza

Kijana ‘fupi nono round’ amshtaki naibu gavana

adminleo