'Timu za mashinani hukuza wanasoka mahiri duniani kama Victor Wanyama'
Na JOHN KIMWERE
KENYA ni miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa wa vipaji vya michezo mbali mbali lakini ukosefu wa ufadhili hufanya vijana wengi, wavulana kwa wasichana kugeukia masuala yasiona na msingi maishani mwao.
Hata hivyo timu za wachezaji chipukizi zinazidi kubuniwa kila uchao huku waanzilishi wakipania kufanikisha malengo tofauti hasa kuwaepusha dhidi ya matendo maovu mitaani.
”Timu za mashinani ndizo hukuza wanasoka mahiri duniani kama Victor Wanyama na Michael Olunga kati ya wengine wengi,” kocha wa Tico Raiders, Reagan Ondeche anasema na kuongeza kuwa wachezaji wa miaka ya sasa hushiriki soka wakiwa na ndoto ya kutinga kiwango cha kuzipigia klabu mahiri katika mataifa ya bara Ulaya.
Tico Raiders ambayo hupatikana katika mtaa wa Kiambiu ni miongoni mwa vikosi vinavyoshiriki Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 msimu huu.
Kocha huyo anadokeza kuwa ingawa kikosi chake hakina mfadhili ana imani atasaidia wengi kupata ufadhili wa masomo angalau kujijengea maisha ya baadaye.
”Kiambiu inapatikana katika mitaa ya Eastlands jijini Nairobi ambayo huorodheshwa kati ya maeneo yenye idadi kubwa ya visa vya uhalifu. Lakini juhudi za wengi wetu kushirikisha vijana katika michezo inazidi kubadilisha mitazamo ya mitaa husika,” alisema.
Katika mpango mzima Tico Raiders inayoshiriki ngarambe ya KYSD kwa mara ya pili msimu huu imepania kumaliza kati ya tatu bora kinyume na ilivyokuwa muhula uliyopita ilipoibuka ndani ya kumi bora.
”Bila kujipigia debe MASA, Sharp Boys na bingwa watetezi, Kinyago United ndizo timu zinazotetemsha chipukizi wangu,” alisema na kuongeza kuwa vituo kama KYSD vinahitaji wadhamini kuzipiga jeki ili kuendeleza mipango ya kupalilia vipaji vya wachezaji chipukizi mashinani.
Ingawa Tico Raiders inashikilia nafasi ya sita kwa alama 13, kocha huyo analenga kuibuka kati ya nafasi tano bora mwishoni mwa mechi za raundi ya kwanza ili kwenye kampeni za mkumbo wa pili wapiganie kutimiza azma yao.
Tico Raiders inajumuisha chipukizi kama: Brandon Otieno (nahodha), Denzel Okoth, Farzal Onyango, Grandton Otieno, Fidel Omondi, Byrone Opiyo, Samson Koye, Marvin Ndemo, Felix Ochieng, Gevan Owino, Rayte Otieno, David Wanjala na Warick Otieno.
Tico Raiders inajivunia kushiriki na kumaliza katika nafasi bora kwenye mashindano tofauti tangu ianzishwe mwaka 2013. Inajivunia kumaliza ya nne mara mbili mechi za Mazingira Cup pia Mpira na masomo mwaka 2017 na 2019 mtawalia.
Aidha mwaka 2017 iliibuka ya tatu baada ya kubanduliwa kwenye nusu fainali shindano la Kilume Memorial Cup.
Michuano ya KYSA imekuza wachezaji wengi akiwamo Brian Opiyo na Bixente Otieno (MASA), Saidi Musa (Star Soccer Academy), Keith Imbali (Kinyago United) ambaye huchezea Gor Mahia Youth.