• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
Klabu za EPL kupiga abautani kuhusu kufunga kipindi cha uhamisho mapema

Klabu za EPL kupiga abautani kuhusu kufunga kipindi cha uhamisho mapema

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

UINGEREZA ilikuwa nchi ya kwanza kuamua kufunga kipindi chake kirefu cha uhamisho kabla ya Ligi Kuu (EPL) kuanza – na inaonekana itakuwa ya mwisho.

Msimu mmoja tu baada ya kufunga kipindi kirefu cha uhamisho kuliko mataifa mengine ya Bara Ulaya, Uingereza sasa inawazia kutupilia mbali wazo hilo na kufanya kipindi chake kiwe sawa na wenzake.

Mnamo Septemba 7, 2017, klabu za EPL zilipiga kura kufunga soko lao siku moja kabla ya msimu mpya kuanza.

Awali, Uingereza ilikuwa inaruhusu klabu nchini humu kusaini wachezaji hadi Agosti 31.

Wakati huo, klabu 14 kati ya 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza ziliidhinisha soko lifungwe mapema.

Manchester City, Manchester United, Crystal Palace, Watford na Swansea City zilipinga wazo hilo nayo Burnley haikushiriki katika kura hizo.

Ripoti nchini Uingereza sasa zinasema kuwa klabu tatu zilizounga mkono shughuli ya kununua wachezaji ifungwe mapema nchini Uingereza zinataka mabadiliko ili zilijiuepushie madhara ya kukosa kununua vizibo klabu nje ya EPL zinaponunua wachezaji wao.

Suala la kujadiliwa

Gazeti la Telegraph nchini Uingereza lilisema Jumatatu, Septemba 2, 2019, kuwa suala hili sasa litakuwa mezani wakati viongozi wa klabu watakutana Septemba 12.

“Hata hivyo, kura ya mipango ya msimu 2020-2021 huenda ikaahirishwa hadi Novemba mwaka 2019,” gazeti hilo limeongeza.

Kipindi kirefu cha uhamisho cha Uingereza cha mwaka 2019 kilifunguka Mei 17 na kufungwa baada ya wiki 12 mnamo Agosti 9.

Kilitamatika wiki mbili na nusu kabla ya mataifa mengine ya Bara Ulaya kukamilisha shughuli hiyo hapo Septemba 2.

You can share this post!

Van Dijk mbioni kushinda tuzo ya mwanasoka bora duniani

Kilimo cha kuzalisha mapapai

adminleo