Michezo

Waterworks inavyojiandaa kupepeta wapinzani

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

KIKOSI cha Waterworks kimezamia maandalizi ya kujiweka vizuri kushiriki michuano ya kuwania taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.

Meneja wake, Fredrick Omondi anasema wanaendelea kuweka mikakati sawa kuhakikisha kuwa timu hiyo itafanikiwa kuteremsha ushindani wa nguvu kwenye migarazano ya kipute hicho.

Ofisa huyo anasadiki kuwa kama desturi yao vijana wake watakwenda kushindana wala siyo kushiriki tu hali inayotarajiwa kushuhudia ushindani mkali. Bila shaka wachezaji wa kikosi hicho wameendelea kutamba kwa kuzingatia wamepandishwa daraja msimu mmoja baada ya kupanda walipoibuka wafalme wa Ligi ya Kaunti ya Nairobi.

Msimu uliyopita maofisa wa kikosi hicho walinukuliwa wakisema kwamba wamepania kuendeleza mtindo wa kufanya kweli bila kushiriki ligi yoyote kwa zaidi ya muhula mmoja.

Katika mpango mzima meneja huyo anafichua kuwa wamezamia shughuli za kukipanga kikosi hicho hasa kunasa huduma za wanasoka wapya ili kujiongezea nguvu kwenye jitihada za kufukuzia ubingwa huo.

”Lazima tusajili wachezaji kadhaa ili kuchochea wenzao ligini maana soka la Kenya linazidi kuimarika kila uchao bila kusahau michezo ya Daraja la Pili iko juu kinyume na ilivyo katika kipute cha NWRL,” akasema.

Baadhi ya vijana wa Al Swafaa FC walioshiriki kipute cha NWRL. Picha/ John Kimwere

Waterworks FC na South B Sportiif FC zitashiriki kampeni za ngarambe hiyo baada ya kumaliza katika nafasi mbili za kwanza kwenye michezo ya Nairobi West Regional League (NWRL) msimu uliyoipita.

Wachana nyavu wa Waterworks chini ya kocha, Anthony Nderitu walitwaa ubingwa wa taji hilo walipobwaga South B Sportiff FC kwa goli 1-0 katika fainali iliyopigiwa Ugani Kenya School of Government (KSG) Kabete, Nairobi.

Wanasoka wa pande zote walizua upinzani mkali wakiwinda kutawazwa mabingwa wa taji hilo ambapo Waterworks FC ilifaulu kuibuka wakali ilipofuma goli la ushindi kupitia juhudi zake Vitalis Okomo dakika ya 80.

”Nashukuru wenzangu kwa kuonyesha ushirikiano mwema katika patashika hiyo maana haikuwa mterembo kwani wapinzani wetu kiasi walionekana kutulemea,” nahodha wa Waterworks, Zuberi Mohamed alisema na kuongeza kuwa baada ya ufanisi huo sasa wanageukia michezo ya hadhi ya juu.

Waterworks FC ilishiriki mchezo huo baada ya kuibuka kidedea kwenye mechi za Kundi A kwa alama 27 ikiwa ushindi wa mechi saba, kutoka nguvu sawa mara sita na kudondosha patashika moja. Nayo Kenya Prisons ilimaliza mbili bora kwa kuzoa pointi 24 sawa na Al Swafaa FC pia Riruta United (Makarios 111) FC tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Wanasoka wa Waterworks FC na viongozi wao. Picha/ John Kimwere

Kwenye michuano ya Kundi B, South B Sportiif FC ilimaliza ya kwanza kwa kufikisha pointi 27, moja mbele ya majirani zao South B Allstars.

South B Sportiff FC ilifanikiwa kushinda mechi nane, kutoshana nguvu mara tatu na kuyeyusha mechi tatu. Nao chipukizi wa AFC Leopards walifunga tatu bora kwa kukusanya alama 20.

Naibu kocha wa Waterworks, Josiah Okello anasema “Bila shaka tunafahamu kuwa kampeni za Daraja la Pili kamwe siyo rahisi tunatarajia kukabili ushindani mkali baina ya washiriki wengine ambapo baadhi yao wamecheza kiwango hicho kwa misimu kadhaa.”

Kikosi hicho kimeundwa na wanasoka ambao wengi wao wamekuwa wakisakatia Ulinzi Stars ya Ligi Kuu ya KPL nchini.

Waterworks FC inaonekana inakwenda kwa kasi kama ilivyo kwa wanawake wa Kahawa Queens katika mchezo huo nchini. Inabainika kuwa wachezaji wa vikosi hivyo wanakula fiti pia hushiriki mazoezi ya pumzi na stamina ili kujiweka vizuri kugaragaza gozi ya ng’ombe.