Hofu ratiba ngumu ya AK itaathiri Kenya jijini Doha
NA CHRIS ADUNGO
INGAWA wanariadha waliowakilisha Kenya kwenye Michezo ya Afrika (AAG) jijini Rabat, Morocco mwaka 2019 walijitwalia medali 10 za dhahabu, saba za fedha na tatu za shaba, kikosi hicho kiliambulia pakavu katika mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanaume na wanawake.
Kulingana na kocha Julius Kirwa, ilikuwa vigumu kwa Kenya kutawala mbio hizo hasa ikizingatiwa ufupi wa muda uliokuwepo kati ya kipindi cha kuteuliwa kwa kikosi na kuandaliwa kwa mashindano yenyewe.
“Tulifahamu uzito huu katika mbio za kilomita 10. Waliotuwakilisha walikuwa wanariadha wale wale tu walioshiriki mchujo wa kitaifa wa kufuzu kwa Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar siku nne kabla ya kufunga safari ya kuelekea Morocco. Hivyo, hapakuwapo na muda wa kutosha kwa watimkaji kupumzika,” akasema Kirwa.
Baada ya kuwasili nchini kutoka Rabat, wanariadha wa Kenya sasa wana wiki moja pekee ya kujiandaa kwa mchujo wa kitaifa utakaotumiwa kuteua kikosi kitakachonogesha Riadha za Dunia kati ya Septemba 28 na Oktoba 6, 2019.
Mchujo wa kitaifa umeratibiwa kufanyika mnamo Septemba 12-13 uwanjani Nyayo, Nairobi. Katika michezo ya AAG, baadhi ya wanariadha wa Kenya, akiwemo Conseslus Kipruto ambaye ni bingwa wa dunia na olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi walijiondoa mbioni wakilalamikia majeraha na maumivu ya kila sampuli, jambo ambalo kwa sasa Kirwa ametaka Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kulishughulikia.
Msimu huu umekuwa mgumu zaidi kwa wanariadha wa Kenya walioanza ratiba ya AK kwa mchujo wa kufuzu kwa Mbio za Nyika za Dunia jijini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30.
Mchujo mwingine
Baadaye, kulikuwa na mchujo mwingine wa kutafuta kikosi kilichoshiriki Mbio za Dunia za kupokezana vijiti jijini Yokohama, Japan mnamo Mei 11-12.
Kukamilika kwa mbio hizo kulipisha riadha za kitaifa zilizoandaliwa Nyeri, Mumias na Narok kati ya Mei 4 na Juni 8 kabla ya kufanyika kwa mchujo wa AAG uwanjani MISC Kasarani mnamo Juni 20-22.
Mchujo wa kitaifa kwa wanariadha zaidi walioshiriki AAG uliandaliwa jijini Nairobi kati ya Agosti 20-22 huku baadhi ya walioteuliwa wakielekea Morocco siku moja baadaye.