SHANGAZI AKUJIBU: Nina kipusa akiguswa tu jamani anasalimu amri!

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimegundua mwanamke mpenzi wangu ana udhaifu mkubwa na hatari. Hawezi kabisa kudhibiti hisia zake na nisipokuwa naye akiguswa na mwanamume kidogo tu anawaka moto na kusalimu amri. Nampenda sana lakini kasoro yake hiyo inanitatiza. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninajua kuwa kuna watu, wanaume kwa wanawake, ambao hawawezi kudhibiti hisia zao. Hiyo ni hali ya kimaumbile na sidhani kuna dawa ya kuitibu. Ingawa unasema unampenda, ni wazi kuwa hutawahi kuwa na amani kwani unajua kwa hakika kuwa usipokuwa karibu naye anaweza kunaswa kwa urahisi na mwanamume yeyote. Tathmini wazo hilo na ufanye uamuzi unaofaa.

 

Nataka kuolewa tena

Vipi shangazi? Tuliachana na mume wangu miaka miwili iliyopita na hajawahi kunipigia simu wala jamaa yake yeyote kuniuliza kilichotokea kati yetu. Pili, hakuwa amenilipia mahari wala wazazi wake hawajui kwetu ilhali tulikuwa tumeishi pamoja kwa miaka mitano. Je, nikiolewa kuna shida?

Kupitia SMS

Sidhani mwanamume huyo ana haja nawe kama hajawasiliana nawe katika miaka miwili hiyo. Nashangaa pia kwamba ulikubali kuishi naye kama mke wake kwa miaka mingi namna hiyo na hukushughulika kuhalalisha ndoa yenu. Hutakosea kwa kuolewa kwa sababu ndoa yenu haikuwa halali kwani hajakulipia mahari.

Kumbe ameoa!

Shikamoo shangazi! Kuna kijana ambaye tumekuwa wapenzi na hatujawahi kukosana tangu tulipojuana, hata tulikuwa tumepanga kuanza maisha pamoja hivi karibuni. Juzi nilimpigia simu nikitaka tuonane akaniambia hayuko karibu. Nilishuku ananihadaa kwa hivyo nilitaka aniambie ukweli ndipo akanitumia SMS kuniambia ameoa. Hatua yake hiyo imeniacha hali mbaya hata maisha hayana ladha. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hatua yake hiyo ilikuwa ya ghafla na ndiyo maana imekuacha kati hali hiyo. Ninaelewa unapitia kipindi kigumu lakini nakushauri ujipe moyo na kukubali ukweli kwamba uhusiano kati yenu umekwisha kwani mwenzako ameoa. Muda si mrefu hali hiyo itatoweka na uweze kuendelea na maisha yako.

 

Nafikiria kumuacha ila sijui nianzie wapi

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 22 na nimekuwa na mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miezi minane. Ameniahidi kunioa lakini nimegundua bado amekuwa akiwasiliana na mpenzi wake wa awali. Nilimuuliza akasema uhusiano wao wa kimapenzi uliisha lakini bado ni marafiki. Nafikiria kumuacha lakini kwanza naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Watu waliowahi kuwa wapenzi na wakaachana wanaweza kuendelea kuwa marafiki. Hata hivyo, huwa kuna hatari yao kurudiana hasa kama wanakutana mara kwa mara. Sababu ni kuwa hisia huwa bado zipo na wakisahau kilichowafanya waachane watajipata pamoja tena. Haitakuwa makosa kumwekea mpenzi wako sharti kwamba akome kuwasiliana na mpenzi wake wa awali kama anataka muendelee.

 

Anataka uhusiano lakini tayari amezaa watoto wawili

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke fulani ambaye anataka tuwe na uhusiano lakini ana watoto wawili wa mwanamume aliyekuwa mpenzi wake. Nishauri.

Kupitia SMS

Unavyoeleza ni kama kwamba yeye ndiye anayekutaka na wewe humtaki labda kwa sababu ana watoto. Iwapo mtakuwa na uhusiano au la itategemea wewe mwenyewe. Kama wewe pia unampenda sidhani watoto watakuwa kikwazo.

 

Nitaepuka vipi kupachikwa mimba?

Kwako shangazi. Huu ni mwaka wa pili tangu nilipoanza uhusiano na mwanamume tunayefanya kazi pamoja. Sasa tumeamua kuwa wakati umefika wa kufurahia mahaba. Nahitaji ushauri kuhusu jinsi bora ya kuepuka mimba.

Kupitia SMS

Kuna kinga aina mbili ambazo ni maarufu. Kuna kondomu na pia kuna dawa za kutumia ili kujikinga na mimba. Ukichagua kutumia dawa, itabidi umuone mtaalamu wa afya ya uzazi ili akushauri kuhusu dawa unazofaa kutumia na jinsi ya kuzitumia.

Habari zinazohusiana na hii