VITUKO: Sindwele peku hadi kwa Pengo kumshtakia usaliti wa Simba
Na SAMUEL SHIUNDU
SINDWELE alijuta na kufedheheka kila nukta.
Aliwalaani Asumini na Simba kwa kumsababishia mazonge yaliyokuwa yakimwandama sasa.
Aliamini kwamba wajalaana wale wasingempotezea muda, asingekuwa na tatizo la usahihishaji wa mtihani ambao sasa ulimzulia kiherehere shuleni Bushiangala.
Kila wakati alikuwa anaandamana na Simba kwenda kumwona Asumini.
Alimtekelezea mkubwa wake wa kazi jukumu hili la ushenga hadi siku ile alipofurushwa na Asumini. Siku hiyo ilimdhihirikia kuwa kwa wawili hawa alikuwa kopo la msalani ambalo hutelekezwa baada ya haja kutimizwa.
Alimpata Pengo akipumzisha mavune ya muhula uliokuwa umetamatika. “Ushafika kuzisikia habari za Asumini mapema hivi?” Pengo alimtania mwenzake akiinuka kumpokea.
Aliyetaniwa hakurejesha utani kama ilivyokuwa kawaida yake. Alijiinamia na kusawijika kama mfiwa.
Pengo alishuku kuwa kulikuwa na la mno. Akamwelekeza chini ya mwembe mbali na nyumba kulikokuwa na faragha. Wakavikalia viti vya henzirani vilivyokuwa chini ya mti huo.
“Likizo inakupelekaje?”Pengo alimuuliza mwenzake kwa sauti babaifu. Sindwele alishusha pumzi na akaanza kumsimulia mwenzake yaliyompata. Alimweleza kuhusu ushenga aliomtekelezea Simba kwa uaminifu mkubwa. Alimweleza jinsi safari zake za kumtafuta Asumini zilimpotezea muda wake akawa hapatikani tena shuleni jinsi alivyohitajika. “Si unakumbuka jinsi alivyotufurusha kwake eti ywataka kujinafasi?” Sindwele alimkumbusha.
“Nakumbuka pia Simba akikuambia ufanye adabu na kurejea kazini” Pengo alimjuza mwenzake kumdhihirishia kuwa alikumbuka kisa hicho cha kufurushwa.
“Nilirejea kazini nikakutishwa mengine na naibu wa Simba.” Sindwele alitamka na kusita. “Nakusikiliza” Pengo alimhimiza.
Sindwele aliangaza macho yake huku na kule kuhakikisha kuwa hakuna aliyewasikiliza kisha akamnong’onezea mwenzake jinsi alivyokabidhiwa rundo la karatasi za kusahihisha. Akalalamika jinsi alivyoharakishwa kulisahihisha na jinsi kuharakishwa huku kulimsababishia makosa katika usahihishaji. Hakueleza jinsi alivyowapa watahiniwa alama zisizofaa.
Hakueleza kuhusu mwanafunzi aliyetuzwa alama tele kwa majibu ya Kichina kisichoeleweka.
Kwa ufupi, Sindwele alihitaji msaada wa Pengo japo hata mwenyewe hakujua angesaidiwa vipi. “Nahitaji muda kulifikiria suala hili. Usijali rafiki, Mungu atatunusuru na mabaya ya walimwengu” Pengo alimuusia mwenzake. Wakati huo, Felistus aliwaletea chai kwa mahamri ya nazi. Akamuuliza Sindwele habari za Sofia. Sindwele akalalamika kuwa Felistus haji kuwajulia hali. Felistus akaahidi kuwa angeenda kuwaona. Akarejea jikoni.
Sindwele alikitwaa kikombe cha chai na kuyapiga mafunda kadhaa hafifu.
Alisinzilia mahamri kisha akatangaza kuwa alikuwa katosheka. Pengo alimhurumia mgeni wake. Akapendekeza kuwa walipaswa kwenda matembezini ili angaa mwenzake ajisahaulishe na matatizo ya Bushiangala. Wakaenda kumwona Msodai.