HabariSiasa

Nguvu mpya za Raila serikalini

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, amepata nguvu na ushawishi mkubwa serikalini, licha ya kukanusha kwamba ameacha majukumu yake kama kiongozi wa upinzani.

Kwa kila hali, Bw Odinga anaonekana kuwa na usemi serikalini huku akishauriana na maafisa wakuu, wakiwemo mawaziri, wakuu wa idara mbali mbali, mabalozi na kukagua miradi ya maendeleo.

Afisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi, imekuwa kama madhabahu huku akitembelewa na maafisa wa serikali kuu na za kaunti. Isitoshe, amewahi kupokea na kushauriana na kiongozi wa nchi ya kigeni katika afisi hiyo.

Jana, alishauriana na viongozi kutoka kaunti za Kisii na Nyamira walioongozwa na magavana James Ongwae na John Nyangarama. pamoja na seneta wa Kisii Prof Sam Ongeri.

“Viongozi kutoka eneo la Kisii leo walimtembelea kiongozi wa chama @RailaOdinga katika afisi yake Capital Hill ambapo walijadili masuala yenye umuhimu wa kitaifa,” chama cha ODM kilisema kwenye ujumbe wa Twitter.

Wadadisi wanasema kuna kila dalili kwamba Bw Odinga alipata nguvu mpya kufuatia muafaka kati yake ya Rais Uhuru Kenyatta waliotangaza Machi 9 2019.

“Yeye na familia yake waliongezewa walinzi na imekuwa vigumu kwa baadhi ya washirika wake kumtembelea walivyokuwa wamezoea kabla ya muafaka huo,” asema mbunge mmoja wa ODM ambaye hakutaka tutaje jina kwa sababu ya uhusiano wake na kiongozi huyo.

Baadhi ya mawaziri ambao wamemtembelea katika afisi yake au kukutana naye kushauriana ni Peter Munya wa Viwanda, Profesa Margaret Kobia wa Utumishi wa Umma, Mwangi Kiunjuri wa kilimo na James Macharia wa uchukuzi.

Aidha, amekuwa akishirikiana na waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i, waziri wa michezo Amina Mohammed na waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa.

Katika kile kinachoashiria kwamba anashawishi maamuzi ya serikali, Bw Odinga amekuwa akitoa matamshi ya kuunga sera za serikali na kila anakoenda, anapokewa kwa heshima zote za afisa wa serikali.

Wadadisi wanasema sio siri kwamba Bw Odinga anafahamu, kushawishi au kuhusika na maamuzi ya serikali tangu muafaka wake na Rais Kenyatta.

“Amekuwa akiweka wazi kuwa yeye na Rais Kenyatta waliamua kushirikiana kufanikisha ajenda na sera za serikali. Amenukuliwa mara kadhaa akisema yeye na Rais Kenyatta wameamua kupigana na ufisadi. Mtu hawezi kufanikisha ajenda za serikali akiwa nje ya serikali,” asema mdadisi wa siasa, Duncan Wafula.

Kulingana na Bw Munya, mawaziri wanashauriana na Bw Odinga kwa sababu ya ushirikiano wake na Rais Kenyatta wa kuunganisha Wakenya.

“Wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga walizindua kamati ya uwiano (BBI), ilikuwa ishara kwamba tunapaswa (mawaziri) kushirikiana na Bw Odinga kwa sababu hata yeye ni Mkenya,” Bw Munya aliambia Taifa Leo baada ya kuzuru Urusi akiwa na Bw Odinga.

Mawaziri wote waliagizwa kushirikisha BBI katika ajenda za serikali ishara kuwa wanapaswa kumtambua na kushirikiana na Bw Odinga.

Kulingana na msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango, kiongozi huyo wa ODM, hana wadhifa wowote serikalini lakini maafisa wakuu huwa wanatafuta ushauri kutoka kwake hasa kuhusu masuala anayoelewa vyema kama miundomisingi.

Mnamoi Julai, Bw Odinga alizuru maeneo yanayojengwa vituo maalumu vya kiuchumi jijini Kisumu akiwa na Waziri Macharia. Wiki jana, alizuru mradi wa kilimo wa Galana Kulalu akiandamana na maafisa wa serikali.

Ametumia mamlaka yake kuhakikisha ngome yake ya Nyanza na hasa jiji la Kisumu imepata maendeleo tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza cha utawala wa Jubilee.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale alishangazwa na jinsi Bw Odinga anashawishi serikali kuzindua miradi ya maendeleo Nyanza.

Aidha, wanachama wa ODM wameteuliwa katika bodi za mashirika ya serikali akiwemo afisa mkuu mtendaji wa uliokuwa muungano wa NASA Norman Magaya (bodi ya kudhibiti filamu) na mwanaharakati wa ODM David Osiany (Bodi ya kampuni ya sukari ya Chemelil).

Katika ziara zake nje ya nchi, Bw Odinga amekuwa akipokewa na mabalozi wa Kenya na kupewa heshima zote za kiongozi wa serikali tofauti na awali alipozuiwa kutumia eneo la watu mashuhuri katika viwanja vya ndege nchini.

Hali ni sawa anapozuru maeneo tofauti ambapo amekuwa akipokewa na makamishna wa kaunti na usalama kuimarishwa. Magavana wengine ambao walimtembelea ni Ann Waiguru wa Kirinyaga, Granton Samboja wa Taita Taveta na Alfred Mutua wa Machakos.