Seneti yaridhia mgao wa Sh316.5 bilioni za kaunti 47
Na DAVID MWERE
SENETI imebadili msimamo wake wa awali wa kuwapinga wabunge kuhusu mgao wa fedha za kutoka kwa serikali kuu hadi zile 47 za kaunti.
Alhamisi mchana, maseneta wamehiari kuchukua Sh316.5 bilioni zilizo kwenye nakala mpya ya Mswada wa Ugavi wa Raslimali ambao ungali kwenye kamati ya mazungumzo baina ya bunge la seneti na bunge la kitaifa.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen amesema wamefikia uamuzi huo mgumu ili kunusuru serikali za kaunti ambazo kupitia kwa baraza la magavana zilitishia kufunga shughuli mwezi huu wa Septemba.
Magavana wamekuwa wakitaka wapewe takribani Sh335 bilioni.