• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
AK yatafuta suluhu ya mbio za mita 10,000

AK yatafuta suluhu ya mbio za mita 10,000

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei amefichua kwamba shirikisho hilo litandaa kikao maalumu na watimkaji wa kiume watakaowakilisha Kenya katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 28 na Oktoba 6, 2019.

Kwa pamoja na Julius Kirwa ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya riadha, wawili hao wamesisistiza kuwa hatua hiyo inachochewa na kudorora pakubwa kwa makali ya wanariadha wa Kenya katika fani hiyo kwenye mashindano mengi ya haiba kubwa duniani.

Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio hizo katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo ambayo imekuwa ikitamalakiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah wa Uingereza kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hata kwenye Michezo ya Olimpiki haijawa ya kuridhisha katika miaka 30 iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988.

Tuwei na Kirwa wanahisi kwamba kikao na wanariadha wanaoshiriki mbio hizo huenda kikafichua tatizo lililopo na hivyo kuwachochea wadau kulishughulikia wakati Kenya inapojiandaa kunogesha Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar.

“Hakika, mbio za mita 5,000 ni fani ambayo imekuwa ikiwaumiza vichwa mashabiki, wanariadha na vinara wa AK kwa kipindi kirefu. Naamini kwamba kikao na wadau wa mbio hizo kitatupa jukwaa mwafaka la kulizamia tatizo hilo kwa kina na kuibuka na suluhu ya kudumu ambayo itashuhudia ufufuo wa Kenya katika fani hii ambayo kwa sasa inatawalia na Waethiopia,” akasema Kirwa.

Kulingana naye, kikao hicho kikaandaliwa mwishoni mwa mchujo wa kitaifa utakaofanyika uwanjani Nyayo, Nairobi kati ya Setptemba 12-13, 2019. Mchujo huo utatumiwa kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya nchini Qatar.

Wito wa AK unajiri wiki chache baada ya Geoffrey Kamworor, 26, kufichua kwamba hatakuwa sehemu ya kikosi cha Kenya kitakachoshiriki Riadha za Dunia.

Watimkaji wanaotazamiwa kutoa ushindani mkali jijini Doha na kuwakilisha Kenya ipasavyo katika mbio za mita 10,000 wakati wa Riadha za Dunia baadaye mwezi ujao ni chipukizi Rhonex Kipruto na Rodgers Kwemoi aliyeibuka mfalme wa dunia kwenye mbio za dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 katika mita 10,000 mnamo 2016.

Mwingine atakayekuwa sehemu ya kikosi hicho nchini Qatar ni mwanaridha wa masafa marefu Alex Oloitiptip wa KDF.

You can share this post!

Seneti yaridhia mgao wa Sh316.5 bilioni za kaunti 47

Tabia uchwara zinazoshusha maana halisi ya heshima mazishini

adminleo