Michezo

Kocha hana hofu Stars ikikabili UG bila nyota wanne

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya kuzikosa huduma za viungo Victor Wanyama, Johanna Omollo na beki Joseph ‘Crouch’ Okumu, Harambee Stars watalazimika pia kuyakosa maarifa ya difenda Ismael Gonzalez dhidi ya Uganda Cranes wikendi hii uwanjani MISC Kasarani.

Gonzalez anayepiga soka ya kulipwa kambini mwa UD Las Palmas inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uhispania anakuwa mchezaji wa hivi karibuni zaidi kuthibitishwa na kocha Francis Kimanzi kuwa hatashiriki mchuano huo wa kupimana nguvu.

Kwa mujibu wa Ken Okaka ambaye ni afisa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Gonzalez alipoteza mzigo na stakabadhi zake za usafiri katika uwanja wa ndege jijini Madrid, Uhispania akiwa safarini kuja Nairobi.

“Tulipokea simu kutoka kwa Gonzalez na akaeleza masaibu aliyokumbana nayo safarini. Itamwia vigumu kuwa sehemu ya kikosi cha Stars kitakachovaana na Uganda,” ikasema sehemu ya taarifa ya FKF.

Kukosekana kwa Gonzalez ambaye alitambisha Kenya katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri kunamweka Kimanzi katika ulazima wa kutegemea sasa maarifa ya Johnstone Omurwa wa klabu ya Wazito FC.

Wanyama aliachwa nje ya kikosi cha Stars ili kushughulikia masuala ya uhamisho kati yake na Tottenham Hotspur ya Uingereza iliyokuwa radhi kuzinadi huduma zake hadi Club Brugge ya Ubelgiji au Celtic nchini Scotland.

Kwa upande wao, Omollo anauguza jeraha huku Okumu akihitaji muda zaidi wa kuzoea mazingira kambini mwa waajiri wake wapya IF Elfsborg wa Uswidi waliomsajili kutoka Real Monarchs ya Amerika.

Licha ya nyota hao wanne kutokuwepo katika timu ya Stars, Kimanzi amesisitiza kwamba anajivunia chipukizi wengi wa haiba ambao kwa sasa wana fursa ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo walionao uwanjani.

“Sidhani kwamba hili ni pigo kubwa kwa Stars. Ingawa kila kocha huhitaji wachezaji wake wote bora, hakika sababu za kutokuwepo kwao zinaeleweka,” akatanguliza Kimanzi ambaye mchuano dhidi ya Uganda utakuwa wake wa kwanza kusimamia tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Mfaransa Sebastien Migne aliyetimuliwa na FKF.

“Ni fursa nzuri kwa wachezaji wengine kuvalia jezi za timu ya taifa na kuonyesha utajiri wa vipaji wanavyojivunia,” akaongeza.

Kutokuwapo kwa Wanyama kunamsaza Lawrence Juma wa Gor Mahia kuwa kizibo cha nahodha huyo wa timu ya taifa. Juma anakuwa mchezaji wa tatu baada ya Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars na Bernard Otieno wa Bandari FC kujumuishwa katika kikosi cha Stars hivi karibuni.

Stars watapania kutumia mchuano huo kama sehemu ya mikakati ya kujiandaa kwa kivumbi cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 nchini Cameroon. Kwa Uganda, mechi hiyo itawapa jukwaa la kujinoa kwa mchujo wa mikondo miwili ya kufuzu kwa CHAN 2020 dhidi ya Burundi na AFCON 2021.