Gozi na Cranes litakuwa gumu, wadau waonya
Na CECIL ODONGO
IKIWA imesalia siku moja tu kabla ya mechi kali ya kirafiki kati ya Harambee Stars na Uganda Cranes kusakatwa, wadau mbalimbali wamekiri kwamba vijana wa nyumbani watakuwa na mlima wa kukwea ili kupata ushindi kwenye mtanange huo.
Mkufunzi wa Tusker, Robert Matano alisema Alhamisi kuna uwezekano mkubwa Uganda watatamba kutokana na tajriba na ubora wa timu ya taifa hilo ikizingatiwa Harambee Stars bado ipo kwenye mkondo wa kukijenga upya kikosi chake.
“Sitashangaa iwapo Uganda watashinda mechi ya Jumapili kwa sababu kwa sasa wana kikosi bora zaidi kuliko Harambee Stars. Kenya kwa sasa inaendelea kujenga upya kikosi chake chini ya kocha mpya Francis Kimanzi,” akasema Matano.
Mkufunzi huyo aliongeza kwamba kikosi cha sasa cha Uganda ni imara kwa sababu kinawahusisha wanasoka ambao wamecheza pamoja kwa muda mrefu na wanaoelewana vyema uwanjani.
Hata hivyo, Matano alikariri kwamba anatarajia mchuano mgumu kati ya timu hizo mbili na kuomba Stars kutumia vyema uwanja wa nyumbani kupata angalau sare.
“Hii mechi itakuwa kama debi. Ingawa Uganda ni timu ngumu, Kenya pia itajikakamua na kupigana vikali ikizingatiwa watakuwa nyumbani. Hii itakuwa mtanange wa kusisimua,” akaongeza.
Kauli ya Matano iliungwa mkono na kiungo wa Harambee Stars Francis Kahata, ambaye alikiri kwamba watakuwa na kibarua kigumu kuzima Cranes inayonolewa na Mfaransa Sébastien Serge Louis Desabre.
“Kwa kweli Uganda Cranes ni timu ambayo imeimarika sana katika miaka michache iliyopita. Kwa sasa ni timu nzuri ambayo tutakuwa na kibarua kigumu kuikabili mnamo Jumapili. Walifanya vyema sana kwenye mechi za Mataifa Bingwa Afrika nchini Misri kwa kutinga 16 bora,” akasema Kahata.
Kuondoa uoga
Hata hivyo, Kahata ambaye sasa anasakatia Simba SC ya Tanzania baada ya kuikacha Gor Mahia amewataka wenzake kikosini kuondoa uoga na kukabili mtihani wa Jumapili kwa ujasiri mkubwa. Vilevile amewarai mashabiki kujaza uga wa Kasarani kushangilia timu ya taifa ili ipate matokeo bora.
Mshambulizi tegemeo Michael Olunga pia alikiri kwamba itakuwa kibarua kigumu kukabili Uganda Cranes ila akasisitiza kwamba wachezaji watakaowajibishwa uwanjani watajituma na kulenga ushindi.
“Itakuwa mechi ngumu lakini sisi tutalenga kupata ushindi,” akasema Olunga. Tangu 2015, Uganda haijawahi kushinda Kenya kwa kuwa imepoteza mara moja na kusajili sare mbili.