Semenya abadili kazi, sasa yeye ni mwanasoka
Na MASHIRIKA
BINGWA mara mbili wa mbio za mita 800 kwenye michezo ya Olimpiki, Caster Semenya ameanza kujiandaa kwa maisha mapya nje ya riadha baada ya kujiunga na klabu moja ya soka ya wanawake.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa anakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Kusikiza kesi za michezo (CAS) iliyoidhinisha matumizi ya sheria za Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) zinazotaka wanawake walio na homoni za juu za ‘testosterone’ kutumia dawa kuzipunguza kabla ya kushiriki mashindano yoyote.
Semenya hawezi kutetea taji lake la dunia la mbio za mita 800 jijini Doha nchini Qatar baadaye mwezi huu bila ya kutumia dawa za kupunguza homoni hizo, kitu ambacho amekataa kufanya.
Gazeti la Guardian lilisema Ijumaa kuwa raia huyo wa Afrika Kusini ameanza kufanya mazoezi na klabu ya JVW FC kutoka mjini Gauteng akinuia kusakata mechi yake ya kwanza msimu ujao kwa sababu wakati huu kipindi cha kusajili wachezaji kimefungwa.
“Nachukua fursa hii kwa mikono miwili na ninafurahia upendo na uungwaji mkono ambao tayari nimepata katika timu hii,” gazeti hilo limemnukuu akiambia tovuti ya klabu hiyo.
“Nasubiri kwa hamu kubwa kuanza safari hiyo mpya na natumai nitachangia kadri ya uwezo wangu katika klabu hii.”
Mwanzilishi wa klabu hiyo Janine Van Wyk, ambaye pia ni nahodha wa timu ya Afrika Kusini, alisema, “Ni heshima kubwa kuwa kutoka klabu zote duniani, amechagua JVW kama klabu angependa kuanza kuonyesha ujuzi wake wa soka. Nilimkaribisha katika kipindi cha kwanza cha mazoezi cha timu hii na niliridhika na kuwa ana talanta inayohitajika.”