• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MWANAMKE MWELEDI: Muziki ulifungua milango ya fursa

MWANAMKE MWELEDI: Muziki ulifungua milango ya fursa

Na KEYB

KIBAO chake Kisumu 100 kilimthibitisha kama mmojawapo wa wanamuziki wa kike mahiri nchini ambapo kufikia sasa ana albamu tatu.

Lakini uwepo wake Suzanna Owíyo kwenye ulingo wa muziki, mbali na mdundo wake wa kipekee, ni uhalisi wa muziki wake unaochochewa na mambo ya kawaida, suala ambalo limemuorodhesha miongoni mwa wasanii wanaoheshimika nchini.

Huenda hiyo ni mojawapo ya sababu ambazo zimemzolea tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kora Award na Kisima Award huku akiwahi kuteuliwa katika tuzo za Kora na pia zile za Pearl of Africa Music Awards.

Ni ustadi huu ambao umempa fursa ya kutumbuiza mbele ya marais ikiwa ni pamoja na Hayati Nelson Mandela na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama.

Mwaka wa 2008, Owiyo alikuwa miongoni mwa wasanii wachache waliopewa fursa ya kutumbuiza mbele ya shujaa Mandela kwenye shoo iliyoandaliwa katika eneo la Hyde Park, London, kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 90 tangu kuzaliwa kwake.

Aidha, ametumbuiza katika hafla zingine za haiba ya juu ikiwa ni pamoja na kwenye tuzo za Nobel Peace Prize zilizoandaliwa nchini Norway mwaka wa 2004, kwa heshima yake marehemu Wangari Maathai. Aidha, aliwahi kutumbuiza katika tamasha ya muziki ya MASA Festival iliyoandaliwa jijini Abidjan, Ivory Coast, kando na kushirki kwenye tuzo za Yara Prize Awards mjini Oslo, Norway.

Kutokana na mchango wake katika muziki, mwaka wa 2003, alitawazwa kama mjumbe wa heri njema wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa-UNEP. Na mwaka wa 2011 alipewa tuzo ya the Grand Warrior of Kenya (OGW).

Kabla ya kujiundia jina katika ulingo wa muziki, alifanya kazi kama mpokezi katika saluni, na pia kama kibarua katika kampuni moja katika maeneo ya viwandani jijini Nairobi. Pia, aliwahi kuhudumu kama mcheza densi na bendi kadha za wanamuziki kutoka Congo.

Mzaliwa wa kijiji cha Kasaye, Kaunti ya Kisumu, tangu utotoni, Owiyo alivutiwa na muziki. Kichocheo kikuu kilikuwa kutoka kwa babu yake aliyekuwa mcheza nyatiti. Lakini pia, alivutiwa na wanamuziki wa haiba ya juu kama vile marehemu Miriam Makeba.

Katika umri mdogo alijihusisha na kwaya ya kanisa, vile vile kushiriki katika tamasha za muziki shuleni, na katika harakati hizo kujishindia mataji mengi.

Alikuwa na ndoto ya kutumbuiza jukwaani ambapo angetazama shoo nyingi kwenye televisheni na kuwaiga wanamuziki maarufu.

Baada ya shule ya upili, aliamua kuanza kupiga msasa kipaji chake cha uanamuziki, lakini hilo halikufurahisha familia yake, na hasa babake aliyemtaka awe mwalimu. Lakini pingamizi hili halikumzuia kuandama ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.

Mwaka wa 1998, wakati huo akifanya kazi kama mpokezi katika kampuni ya kakake jijini Nairobi, alisoma tangazo kwenye gazeti kwamba mwanamuziki Sally Oyugi, alinuia kutumbuiza katika hoteli moja jijini.

Owiyo alipiga simu na kuomba kushirikishwa kwenye bendi yake Oyugi. “Aliniambia kwamba angenishirikisha kama mmojawapo wa waimbaji wake, kitu ambacho sikuwa nimewahi fanya,” asema.

Aliimba katika bendi hiyo kwa miaka miwili kabla ya Oyugi kuhamia Amerika, lakini hakumuacha mikono mitupu. “Alinihimiza kuendelea kuimba na kunishauri kwamba nilikuwa na uwezo mkubwa wa kuendelea kimuziki,” asema huku akiongeza kwamba mawaidha hayo yaligeuka kuwa nguzo yake kuu.

Baadaye, alijiunga na bendi kadha za wanamuziki kutoka Congo kama mwanadensi, kabla ya kujiunga na Bora Bora Sound Band mjini Kisumu kama muimbaji.

Safari yake kama mwanamuziki binafsi ilipigwa jeki na kibao chake Kisumu 100 kilichomletea umaarufu na kumshindia mashabiki kibao, na tokea hapo amekuwa akiimarika hatua kwa hatua. Lakini kama wanamuziki wengine mashuhuri, safari yake haikuwa rahisi kwani alipitia milima na mabonde kabla ya kujiundia jina kama mwanamuziki.

Kando na muziki, ameshiriki katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni ya kutetea elimu ya mtoto msichana ya “Because I Am a Girl”.

Mwaka wa 2013, alianzisha ‘Soko Bila aste‘; kampeni inayounga mkono kampeni ya UNEP dhidi ya uharibifu wa chakula.

Mbali na hayo, ameanzisha kituo cha sanaa kwa jina Suzanna Owíyo Trust kwa minajili ya kukuza vipaji.

“Nilitengwa na familia kwa muda kabla yao kukumbatia uamuzi wangu wa kuwa mwanamuziki. Aidha, kupata rasilimali za kunisadia kuendeleza kipaji changu ilikuwa changamoto na kituo hiki kinanuia kuhakikisha kwamba hakuna mtu mwingine anayepitia magumu niliyokumbana nayo,” asema.

Ushauri wa Owiyo ambaye amekuwa akisawazisha majukumu yake kama mama, mke, mwanamuziki na balozi wa heri njema, ni kumakinika. Kulingana naye, ikiwa hangekuwa na ujasiri na uvumilivu, basi asingefika alipo sasa.

You can share this post!

UG yatua nchini kupimana nguvu na Stars kesho Jumapili

SHANGAZI AKUJIBU: Nahofia ataniacha baada ya rafiki yake...

adminleo