TEKNOHAMA: Si lazima vidonge kupanga uzazi
Na LEONARD ONYANGO
HIVI karibuni watu huenda wakaanza kutumia simu zao za mkononi kuzuia mimba zisizohitajika.
Hii ni baada ya majaribio ya kwanza ya programu (app) ya simu kuthibitisha kwamba ina uwezo wa kusaidia familia kupanga uzazi.
Programu hiyo inayojulikana kama Dot Fertility App, ilivumbuliwa na watafiti kutoka Kitivo cha Afya ya Uzazi katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Amerika.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika jarida la kisayansi la European Journal of Contraception and Reproductive Healthcare, apu hiyo hutumia historia kuhusu hedhi ya mhusika kutabiri siku ambazo anaweza kupata ujauzito kisha hutoa taarifa kila siku kwa mtumiaji ikiwa anaweza kupata ujauzito au la.
Majaribio ya kwanza yalithibitisha kuwa inaweza kutoa matokeo sahihi kuhusu uwezekano wa mimba kwa asilimia 95.
Watafiti sasa wanasema programu hiyo itaweza kusaidia kuzuia mimba zisizohitajika sawa na mbinu nyinginezo za kupanga uzazi.
“Tayari baadhi ya wanawake wanatumia apu za simu kupanga uzazi lakini nyingi ya yazo zinawapotosha. Ni sharti ifanyiwe majaribio kutathmini ufaafu wake,” akasema Dkt Victoria Jennings, mkaguzi mkuu ambaye amekuwa akiifanyia majaribio.
“Wanawake wengi wamejipata na ujauzito kwa kutumia apu zinazowapotosha. Hiyo ndiyo maana Dot App inafanyiwa majaribio ya kina ili kuthibitisha kuwa kweli inaweza kutumiwa kupanga uzazi kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa,” akaongezea.
Jumla ya wanawake 718 walijumuishwa katika utafiti huo. Baada ya miezi kadhaa, wanawake 24 walipatwa na ujauzito kwa sababu walipuuza ushauri wa Dot App na kushiriki tendo la ndoa bila kutumia kinga licha ya kuonywa.
Ni mwanamke mmoja tu ambaye alipata ujauzito licha ya kutumia apu hiyo kwa kufuata maagizo kikamilifu.
“Idadi kubwa ya wanawake wanatumia simu na hivyo teknolojia hii huenda ikawa na afueni kubwa kwao kupanga uzazi bila kulazimika kumeza tembe,” akasema Dkt Jennings.
Uvumbuzi huo ulitangazwa siku chache baada ya watafiti kutoka Chuo cha Georgia Institute of Technology, Amerika pia kuchapisha ripoti kuhusu teknolojia inayotumia saa, pete, hereni au mkufu kupanga uzazi.
Kulingana na utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Journal of Controlled Release, watafiti hao waligundua homoni za kuzuia uzazi zinazopakwa kwenye saa, mkufu, hereni au pete.
Homoni hizo huingia mwilini kupitia kwenye ngozi.
Vipimo vya mwanzoni vinaonyesha kuwa homoni hizo zina uwezo wa kuzuia mimba lakini watafiti hao hawajaanza kufanyia binadamu majaribio ili kuthibitisha ufaafu wake.
Majaribio ya kina
Tayari Shirika la Maendeleo la Amerika (USAID) limeanza harakati za kufanyia teknolojia hiyo majaribio ya kina.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFPA) iliyotolewa mwaka jana ilionyesha kwamba wanawake wa Kenya wanaongoza kwa kutumia dawa za kupanga uzazi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kulingana na ripoti ya UNFPA, asilimia 55 ya wanawake walioolewa nchini Kenya hutumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi. Kenya inafuatiwa na Rwanda kwa asilimia 49, kisha Tanzania asilimia 33 na Uganda asilimia 31.
Ripoti hiyo yenye kichwa: Nguvu ya Uamuzi, iliorodhesha Kenya katika nafasi ya tatu barani Afrika baada ya Zimbabwe and Malawi.
Humu nchini, idadi kubwa ya wanawake kutoka eneo la Kati ndio wanaoongoza katika upangaji uzazi.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Performance Monitoring and Accountability (PMA 2020) mwaka jana, asilimia 73 ya wanawake kutoka eneo la Kati wanatumia mbinu za upangaji uzazi.
Eneo la Kati linafuatiwa na Mashariki ambapo asilimia 70 ya wanawake wanatumia dawa za kupanga uzazi na Nairobi (asilimia 63), Bonde la Ufa (asilimia 53), Pwani (asilimia 44) na Kaskazini Mashariki (asilimia 3).
Kaunti ya Kirinyaga ndiyo inaoongoza kwa kupanga uzazi humu nchini kwa asilimia 81, Makueni (asilimia 80), Meru (78), Machakos (76), Tharaka Nithi (74) na Kiambu (74).