Makala

KINA CHA FIKIRA: Gere za Kizungu ndizo zilizofuta hati za Kiarabu na kutulazimishia Kilatini

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

KISWAHILI sanifu kimetufikia kupitia kwa juhudi na njama za Wakoloni.

Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki au Inter-territorial Language Committee iliundwa mnamo 1930 kwa lengo la kuteua lahaja moja miongoni mwa lahaja kadha zilizotanda katika Pwani ya Afrika Mashariki na visiwani iwe ndiyo msingi wa Kiswahili Sanifu.

Jukumu jingine la kamati lilikuwa kubadili hati au orthografia ya kukiandikia Kiswahili.

Kabla kuja kwa Mkoloni, Kiswahili kilikuwa kinatumia hati ya Kiarabu ambayo Wazungu hawakuifahamu wala kuipenda. Hapo ndipo Kamati ya Lugha ilipojukumishwa kubadili hati hadi kuwa ya Kilatini.

Haya masuala ya hati na usanifishaji wa Kiswahili ni tokeo la moja kwa moja la utashi wa Mkoloni kuwa na ushawishi uliopindukia kwa watawaliwa, ushawishi kuhusu kila kipengee cha maisha.

Wakoloni siku zote walidhamiria kudhibiti mwenendo wa maisha ya wale walio chini yao; analalaje, anafikirije, anasemaje, anasema lugha gani, anaisemaje, anaiandikaje, anaionaje?

Mimi nadhani kwamba kauli ya Ngugi wa Thiong’o hapa kuhusu shambulio la kinafsiya dhidi ya Mwafrika katika ‘Decolonizing the Mind’, inasibu hapa.

Kwanza, uamuzi wa kubadili hati au orthografia ulitukosesha wengi wetu umilisi wa ajami uliokuwa umekita mizizi katika matini za Kiswahili.

Hii leo nikitaka kusoma matini za kale za Kiswahili sharti nimtafute Ustadh Mau wa Lamu anayejua kusoma na kuandika hati za Kiarabu.

Maskini mimi wa uwezo wa kusoma baadhi ya kazi za Kiswahili, kwa kweli mbumbumbu sijui ngoma iko wapi.

Nani alisema kile kitu cha Uzunguni kizuri kwetu? Hati za Kiarabu zilikuwa na nakisi gani? Je, zilikuwa haziwezi kubeba sauti za Kiswahili na kuziwasilisha ipasavyo kimaandishi? Sio gere na husuda na chuki za Kizungu zilizoziondoa hati za Kiarabu na kutulazimishia hati za Kilatini?

Tunaweza tukabisha na kusema na vipi hati za Kiarabu, je hizo nazo si shuruti walizopewa Waswahili na wageni wanaotoka Arabuni?

Je, inawezekana kwamba kabla kuja Waarabu, Waswahili walikuwa na hati zao wenyewe za kuandikia lugha yao yenye lahaja tele tele zilizotapakaa katika mwambao wa Pwani na visiwani?

Haya maswali hayawezi kujibiwa vizuri bila kutafakari si tu nani aliamuru kuundwa kwa Kamati ya Lugha, bali pia nani waliteuliwa kuwa kwenye kamati hiyo.

Kumbuka Ujerumani ilikuwa imeipoteza Tanganyika baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na himaya yake kupewa Uingereza.

Ilmuradi eneo zima la Afrika Mashariki lilikuwa himaya ya Uingereza.

Kwa hiyo, ni Mwingireza ndiye aliyeunda Kamati hiyo. Isitoshe, Maamuzi yalikuwa yanafanyika kwenye kamati bila Mwafrika – ambaye yanamhusu moja kwa moja – kuwakilishwa.

Kiunguja cha Unguja mjini ndicho kilichoibuka kidedea. Tokeo ni kutelekezwa kwa lahaja nyingi nyingine zenye ukwasi mkubwa wa msamiati na ushairi kama vile Kiamu, Kimrima, Kimvita na Kipemba.

Hii leo mtoto wa Mombasa anayetahiniwa kwa Kiswahili sanifu akiandika lugha yake anaambiwa hajui Kiswahili. Pema hapo?