Makala

VITUKO: Msodai adamirishwa kwa umero wake, apokea mrapuo mzito toka kwa Sindwele

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL SHIUNDU

KWA wiki mbili sasa tangu shule zifungue kwa muhula wa tatu, Msodai alikuwa kajiinamia kama mfiwa.

Mchana kutwa alishinda kajifungia afisini mwake kama mgonjwa wa ukoma. Alikuwa kapishana na kanuni za uadilifu zilizoiongoza kazi yake ya ualimu.

Mahanjamu na madoido yake ya kawaida yaliota mbawa na kupaa punde tu ziara ya zaraa aliyokuwa kaandaa ilipotibuka. Rafiki zake wa dhati nao wakaanza kumuambaa.

Mmoja wa rafiki hawa wasiojua urafiki wa kufa kuzikana alikuwa mwalimu wa Kiingereza. Madam Ilingish, kama watu wa Bushiangala walivyomuita mwalimu huyu wa Kiingereza alimchukia bwana deputy kwa sababu ndiye aliyepaswa kuandamana naye katika ziara ya zaraa ambayo iliambulia patupu.

Sasa huyu mwalimu Ilingish alianza kusumbuliwa na kile alichokiita uraibu. Wengine lakini walishangazwa na uraibu huu. Haukuwa uraibu wa kawaida.

“Roho inataka mandazi moto!” aliwatangazia wenzake kila walipoletewa chai ya saa nne. Kila alipotangaza hivyo, alifululiza hadi kwenye mkahawa wa shule na kujichukulia mandazi yasiyopungua kumi. Anajali nini? Si anajua mandazi yangegharamiwa na shule? Alikula mandazi mawili tu na hayo mengine akayaweka mkobani. Hayo yakawa mazoea yake mapya kila wakati wa chai.

Masaibu ya Msodai yalimfurahisha Sindwele. Kila siku aliyagusia katika mazungumzo yake. Alimlinganisha Msodai na mwindaji aliyejidhuru kwa mshale wake mwenyewe.

“Msasi mmoja alienda porini kuwinda kama ada yake na pia kwa sababu alikuwa kakabwa na njaa ya nyama.” Sindwele aliwasimulia walimu wenzake. “Msasi huyu alipofika porini, alimwona swara mzuri aliyenona. Akaulenga mshale wake barabara na kuufyatua.

Mshale ulifyatuka fyuu! kuelekea kule kulikokuwa na swara. Kutokana na uchache wake wa subira, msasi yule akaona kwamba mshale ungemcheleweshea windo.

Njaa yamdanganya

Njaa ilimdanganya na kumwelekeza visivyo. Naye akafyatuka kuuandama mshale. Akaufikia na hata kuupiku. Akauacha nyuma na kukimbia hadi akamfikia swara. Vuum! akaukamata mguu wa yule swara. Maskini msasi wetu alisahau habari za mshale uliokuwa nyuma yake. Hatimaye mshale alioufyatua mwenyewe ukampata sawasawa makalioni.”

Waliokisikia kisa hiki waliachilia kicheko. Wote isipokuwa Msodai. Yeye alijua kuwa mchapo huo ulimlenga kwani ndiye aliyekuwa akipanga njama ya kuwaharibia jina Simba na Sindwele.

Ndiye aliyesahau kuwa mchimba kaburi huingia mwenyewe. Aliisahau tamaa yake ambayo baadaye ilimwandama na kumchongea. Aliuchukua mkopo wa m-shwari na kuwarejeshea wanafunzi pesa zao.

Akaapa kuiamsha upya ile kashfa ya Sindwele kutosahihisha mitihani. Laiti angalijua kuwa ushahidi aliotegemea kwa kesi hiyo haukuwepo!