• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Mkondo wa pili wa mashindano ya Victoria Cup kufanyika Nakuru

Mkondo wa pili wa mashindano ya Victoria Cup kufanyika Nakuru

Na CHRIS ADUNGO

MJI wa Nakuru utakuwa mwenyeji wa mchuano wa mkondo wa pili wa Victoria Cup utakaowakutanisha Kenya Simbas na Sables ya Zimbabwe mnamo Septemba 21.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), hatua hiyo ya kimakusudi inalenga kutoa burudani kwa mashabiki wa mchezo huo mashinani na kuwapa wanaraga chipukizi jukwaa mwafaka zaidi la kuchochea vipaji vyao.

Itakuwa mara ya pili mwaka huu kwa mchuano wa haiba kubwa wa raga kuchezewa nje ya jiji la Nairobi baada ya Kisumu kuwa mwenyeji wa mkondo wa kwanza wa kivumbi cha Elgon Cup kati ya Kenya na Uganda mnamo Juni.

Zimbabwe wanaoongoza jedwali kwa alama 17, watashuka ugani kwa minajili ya mchuano huo wakitarajia kuendeleza rekodi nzuri ya kutopigwa katika Victoria Cup hadi kufikia sasa msimu huu. Kenya inashikilia nafasi ya pili kwa pointi 16.

Zimbabwe kualika Zambia

Zimbabwe watakuwa wenyeji wa Zambia wikendi hii, na huenda wakatawazwa mabingwa wa Victoria Cup iwapo watasajili ushindi mnono dhidi ya majirani zao hao.

Uganda ambayo tayari imekamilisha kampeni zake zote katika kipute cha Victoria Cup inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 15 huku Zambia ikikokota nanga mkiani bila alama yoyote baada ya kushindwa kusajili ushindi au sare yoyote kufikia sasa.

Kenya Simbas wataanza mazoezi mwishoni mwa wiki hii chini ya mkufunzi Paul Odera.

“Huu ndio mchuano wetu mkubwa zaidi wa mwisho mwaka huu na tunalenga kukamilisha kampeni kwa matao ya juu zaidi,” akasema Odera.

You can share this post!

Tangatanga wamtishia Mutyambai, wataka Matiang’i...

Riadha: Kikosi cha taifa kuanza kujiandalia Doha

adminleo