• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kupoteza penalti kulimtia Abraham pabaya

Kupoteza penalti kulimtia Abraham pabaya

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MSHAMBULIAJI chipukizi wa Chelsea, Tammy Abraham amedai kwamba mama yake alibubujikwa na machozi kutokana na matusi aliyorushiwa na mashabiki wakati timu yake ilipokuwa ikicheza na Liverpool kwenye fainali ya Uefa Super Cup mwanzoni mwa msimu huu.

Abraham alishindwa kufunga mkwaju wa penalti ambayo ingeiwezesha Chelsea kuibuka washindi wa pambano hilo jijini Istanbul, Uturuki mwezi uliopita, hali ambayo ilichangia shutuma za kila aina katika mitandao ya kijamii dhidi ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 21.

“Nakumbuka nikizungumza na mama yangu. Alikuwa na huzuni sana, huku akilia,” Abraham alisema wakati wa mahojiano na shirika la CNN.

“Alikuwa akifikiria, “kwa nini wamshambulie mwanangu hivi!” Kawaida hakuna mzazi anayeweza kufurahia kabisa wakati mwanawe akirushiwa cheche za matusi. Kwangi, naweza kustahimili. Mambo kama hayo hayanisumbui sana, lakini yanaweza kuvuruga akili za watu wasio na nguvu ya kuvumilia kama mimi,” akasema chipukizi huyo mzawa wa Uingereza.

Siku hiyo, Abraham alibaki amezubaa baada ya kukosa kufunga penalti hiyo. Lakini baada ya kuzungmziwa na maafisa wa kiufundi pamoja na wachezaji wenzake, maisha yalirudi kuwa kawaida.

“Mambo yalienda mrama siku hiyo, lakini lazima watu wakumbuke kwamba mtu yeyote anaweza kupoteza penalti. Namshukuru kocha wangu Frank Lampard kwa kunishauri nilipokuwa nikishutumiwa na mashabiki. Kwa hakika, wakati huo nilihitaji mtu kama yeye kunituliza,” akaongeza.

Kwingineko, Jordan Stevens wa Leeds United amepigwa marufuku ya mechi wiki sita kutojihusisha na masuala ya soka baada ya kuvunja sheri za Shirikisho la Soka la Uingereza (FA). Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, alikiri shtaka la kuwekeza katika mechi 59 tofauti msimu uliopita, tano zikihusu timu yake ya Leeds.Stevens ambaye atakaa bila kucheza hadi Oktoba 10, kadhalika amepigwa faini ya Sh180,000.

“Tumeudhiwa mno na hatua ya FA ya kumwekea mchezaji wetu vikwazo vikali,” alitanguliza Afisa Mkuu wa Leeds, Angus Kinnear.

“Kumzuia mchezaji wa umri mdogo kushiriki soka wakati ligi inaendelea ni adhabu kali kwa mtu ambaye alifanya kitu bila kutarajia,” akaongeza.

Stevens aliyesaliwa kutoka Forest Green mnamo Februari 2018 amepewa nafasi ya kuanza kikosini (Leeds) mara moja pekee tangu atue Elland Road.

You can share this post!

Riadha: Kikosi cha taifa kuanza kujiandalia Doha

Kocha kumpigania chipukizi ambaye anatishiwa maisha

adminleo