Habari

Wakazi wa Makongeni kufurahia huduma bora za usafiri baada ya uzinduzi wa barabara

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wamepata afueni baada ya kukamilika ujenzi wa barabara ya ‘bypass’ ya Posta-Thika-Kamenu-Kiganjo.

Kwa muda wa miezi miwili hivi halmashauri ya kuunda barabara (KERA), kwa ushirikiano na kampuni ya China ya H-Young, wamekuwa wakikarabati barabara kadha za bypass Thika na maeneo  ya karibu.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliyeshuhudia ukarabati wa barabara hiyo ya kutoka Posta ya Thika kupitia Kamenu hadi Kiganjo, alisema Jumatatu wafanyabiashara katika soko kuu la Madaraka, Makongeni watanufaika pakubwa kwa sababu biashara sasa itanawiri kabisa.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina alipozuru soko la Makongeni wakati wa uzinduzi wa Barbara ya Posta Makongeni – Kamenu- Kiganjo mnamo Jumatatu, Septemba 9, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

“Sasa magari mengi yanayoleta chakula yatapita bila shida kwa sababu hakuna matope tena na hayatakuwa yakikwama kila mara,” alisema Bw Wainaina.

Alisema watu wanaofika katika soko hilo kila siku ni karibu 70,000 na kwa hivyo hiyo ni hatua kubwa ya kujivunia.

Alisema jambo muhimu sasa – linalostahili kutekelezwa – ni urekebishaji wa mfumo wa majitaka na kuhakikishi kuwa uzoaji wa taka unadumishwa kila mara ili kuweka mazingira mema katika eneo lote la Makongeni.

“Barabara ni laini na ni sharti tuzingatie tuweke matuta katika maeneo kadha ya barabara yenyewe ili kuzuia ajali za kila mara. Tunaelewa kuwa waendeshaji pikipiki sasa watakuwa na hamu ya kuendesha kwa kasi huku matatu pia zikifuata mkondo huo. Hatutaki kesi za kila mara kwa kuwa watu wanaweza kugongwa na magari; hasa wanafunzi wa shule,” alisema Bw Wainaina.

Kuhudumia watu wengi

Alisema soko hilo la Makongeni linahudumia watu wengi kutoka Machakos, Murang’a, na hata Githurai.

Aliwahakikishia wanaohudumu ndani ya soko hilo kuwa atafanya juhudi kuona ya kwamba wanapata miavuli vya kujikinga kutokana na jua kali.

Bw Stephen Kamau ambaye ni mwenyekiti wa wanabodaboda wa Makongeni Posta, alisema hatua ya barabara hiyo kuundwa imeleta mabadiliko mema kwa sababu hakuna matope watakaoshuhudia tena.

“Hapo kitambo barabara hiyo ilikuwa na mashimo mengi ambapo pikipiki zetu zilipata shida ya kuvunjika vipuri. Hata wahudumu wengi waliwaangusha wateja wao kwa sababu ya mashimo na matope wakati wa mvua,” alisema Bw Kamau.

Naye mhudumu wa teksi Bw Patrick Chege alisema sasa kazi yao itakuwa rahisi ikilinganishwa na hapo awali.

“Kwa zaidi ya miaka 10 tumepata shida kubwa kutokana na gari zetu kupata pancha na kukwama kwenye matope. Sasa mambo yamegeuka na kuwa shwari baada ya barabara hiyo kukarabatiwa,” alisema Bw Chege.