• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
BIASHARA MASHINANI: Wadumishaji usalama waliounda kundi la kilimomseto ili kujikimu

BIASHARA MASHINANI: Wadumishaji usalama waliounda kundi la kilimomseto ili kujikimu

NA CHARLES ONGADI

NI kundi la wadumishaji usalama lililo na mchanganyiko wa wazee kwa vijana katika kijiji cha Mikoroshoni, Shanzu kaunti ya Mombasa linalojihusisha na kilimo mseto.

Naam, Mikoroshoni Community Policing lililoasisiwa miaka 10 iliyopita kwa lengo la kudumisha usalama eneo hili, imekuwa mfano mzuri kwa jamii kwa kujiundia hela kibao kupitia kilimo cha mboga aina ya sukumawiki, Spinachi, biringanya, tomato na mahindi.

Kundi hili la Mikoroshoni Community Policing, limeweza kutumia vyema shamba dogo lilioko katika ofisi za naibu chifu wa Shanzu iliyoko kijiji cha Mikoroshoni kujiinua kiuchumi.

“Tuliamua kujitosa katika kilimo kujiinua kiuchumi bila kuwategemea wakazi wa eneo hili kutulipa kutokana na huduma tunazowapatia za kudumisha usalama,” asema Ngowa Mwaringa Ngowa ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kundi hili.

Ijapo mwanzoni baadhi ya wanachama walisita katika kufikia uamuzi wa kujitosa katika kilimo kutokana na udogo wa shamba, waliukumbatia mara baada ya kupokea ushauri wa kina kutoka wataalam wa kilimo Mombasa.

“Wataalam wa kilimo kutoka ofisi za kaunti ya Mombasa walitupatia ushauri na kutufundisha mbinu aula katika kilimo biashara,” aongeza Mwaringa.

Na katika kuhakikisha kundi hili limepiga hatua katika kilimo, wataalam hao waliwapatia mbegu, mifuko maalum ya plastiki ya kupandia mboga za sukumawiki na mchicha, mbolea na dawa za kuua wadudu.

Cornelius Fondo Omar ambaye ni mwenyekiti wa kundi hili anasema ukosefu wa shamba kubwa uliwalazimisha kutumia mifuko ya plastiki kwa upanzi wa mboga za sukuma wiki na mchicha.

Kilimo hiki kimeweza kuwasaidia wakazi wa kijiji cha Mikoroshoni na maeneo jirani kutosafiri mwendo mrefu hadi soko kuu la Kongowea kununua aina tofauti ya vyakula.

Cornelius Fondo Omar ambaye ni mwenyekiti wa kundi hili anaiambia Akilimali kwamba ukosefu wa shamba umewalazimisha kutumia mifuko ya plastiki kupanda mboga za sukumawiki na mchicha.

Fondo anasema kwamba walianza na mboga za sukuma wiki, Mchicha na Spinachi na baada ya kipindi cha wiki nne wakaanza kuvuna.

Vuno la kwanza liliwawekea mezani kitita cha Sh15,000 na kuwachochea kupanua zaidi kilimo chao kwa kuongeza mimea kama biringanya, nyanya na mahindi.

Kulingana na Fondo, mara hii waliamua kufuata kikamilifu ushauri wa wataalam hao wa kilimo kwa kuongeza rutuba na kukabiliana barabara na wadudu waharibifu.

Ni katika vuno lao la pili ndipo waliweza kutia kibindoni kitita cha Sh60,000 baada ya kipindi cha miezi miwili pekee.

Aidha, Mwaringa anafichulia Akilimali kwamba siri ya mafanikio yao ni kupanda mimea inayochukua muda mfupi kabla ya kuanza kuvunwa. Pia wana kisima cha maji wanayotumia kunyunyizia shamba lao kila asubuhi na jioni wakati wa kiangazi.

Kulingana na Ngowa, mboga kama mchicha na sukumawiki, nyanya na biringani huchukua kipindi kifupi kukomaa na kuwa tayari kuvunwa.

“Tunavuna mboga kwa kipindi cha miezi sita kabla ya kung’oa na kupanda mimea mingine mipya ikiwa ni faida tupu kwetu,” asema Mwaringa.

Bi Kadzo Kalama ambaye ni mkazi wa mtaa wa Keroport anasema kwamba tangu kundi hili lianzishe kilimo chao miaka kadhaa iliyopita, amekuwa akila mboga freshi kila siku.

“Zamani nilikuwa nikinunua mboga vibandani ambazo mara nyingi huwa zimesinyaa baada ya kushinda mchana kutwa kwenye jua kali, lakini katika shamba la Mikoroshoni Communty Policing kila kitu ni freshi tu,” asema Bi Kadzo.

Ngowa Mwaringa na Cornelius Fondo wakionesha mboga za mchicha nasukumawiki walizopanda katika mifuko maaluum ya plastiki katika shamba lao lililoko Keroport, Shazu Mombasa hivi majuzi. Picha/Charles Ongadi

Wateja wengi huwa ni wakazi wanaoishi mitaa ya Mikoroshoni, Shanzu, Utange, Pendua na Maweni wanaonunua kwa matumizi yao ya nyumbani tu.

Wanachama hao wanasema kilimo chao kinalenga kutosheleza mahitaji ya wakazi wa eneo wanalolihudumia kiusalama pekee.

Wasema mara nyingi sisi huwalenga wakazi na wala siyo wafanyabiashara wanaonunua kwa wingi kwa lengo la kulisha jamii yao kwa vyakula freshi.

Mwaringa asema kwamba mbali na kilimo kundi hili pia linajishughulisha na uzoaji wa taka katika maeneo ya Mikoroshoni na wadi ya Shanzu kwa ujumla.

“Awali tulikuwa tukiwategemea wakazi wa kijiji kutulipa kwa kutoa huduma za usalama nyakati za usiku lakini tangu tujitumbukize katika kilimo, tumekuwa tukijitegemea wenyewe,” asema Mwaringa.

Kundi hili la Mikoroshoni Community Policing limeanza mchakato wa kupanua kilimo chao kwa kununua shamba la ekari moja.

Wasema wanashukuru kaunti ya Mombasa chini ya Gavana Hassan Joho kwa msaada wao mkubwa ambao umeweza kuwakwamua kiuchumi.

You can share this post!

RIZIKI NA MAARIFA: Utingo mwanamke aliyejipata katika ajira...

Afueni kwa raia, pigo kwa wabunge Rais kukataa kutia saini...

adminleo