• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Morani anayesuka hela ndefu kwa kusonga nywele

Morani anayesuka hela ndefu kwa kusonga nywele

Na CHARLES ONGADI

SHUGHULI za kawaida zinaendelea huku kila mmoja akionekana akipambana na hali yake katika kusaka mkate wa kila siku katika kituo cha biashara cha Lights, Kengeleni, Mombasa.

Katika upande wa pili wa barabara kuu ya Mombasa/Malindi katika steji ya matatu ya kuelekea Mishomoroni, hapa kuna vibanda vya vyakula na saluni.

Hapa tunamkuta Molel Melio, akichapa kazi yake ya ususi katika kibanda chake kilicho huku wateja kadhaa wakikaa kitako wakisubiri huduma zake.

Molel anavuna hela kibao kutokana na kazi ya kuwasonga nywele akina dada, kazi inayobezwa na vijana wengi wa kiume nchini.

“Hapa ni kazi tu wala hatuna muda wa kuchagua kazi ilimradi tumepata hela ya kutukimu kimaisha,” asema Molel, mzaliwa wa Monduli nchini Tanzania miaka 37 iliyopita.

Siyo Molel pekee anayefanya kazi hii ya ususi inayokisiwa na wengi kuwa inayofanywa sana na akina mama bali wako wasusi wengi wa kiume kutoka jamii ya kimaasai wanaofanya kazi hii.

Kulingana na Molel, hakupitia kituo chochote cha mafunzo ya ususi bali ni mafunzo aliyopitia akiwa morani na wala hakujua kwamba siku moja ingekuwa kitega uchumi kwake.

Mara alipoingia nchini mwaka wa 2007, Molel alibahatika kuajiriwa kama chokodari katika mojawapo ya kampuni za ulinzi mjini Mombasa.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi kwa kipindi cha miaka minne aliamua kuachana na kazi ya kuajiiwa kutokana na malipo duni aliyokuwa akipokea.

“Malipo niliyopokea kama mlinzi wa usiku kamwe hayakuweza kukithi mahitaji yangu muhimu hivyo nikalazimika kuacha kazi hiyo ya kuajiriwa na kuamua kujiajiri,” asema Molel.

Ni kipindi hicho cha kusaka kazi ndipo alipowaona wenzake wakifanya kazi ya ususi eneo la Lights, Kengeleni na mara moja akavalia njuga kazi hii.

Kulingana na Molel, ni kazi ambayo hakuhitaji kufunzwa na yeyote kwa kuwa ni kazi aliyojifunza tangia utotoni kipindi hicho akiwa morani.

“Tukiwa morani tulijifunza mitindo mingi ya kusonga twisti na wala sikujua itafikia wakati nitatumia ujuzi huo kujikwamua kiuchumi,” anaiambia Akilimali wakati wa mahojiano majuzi.

Mtindo wa twisti

Molel anasonga mtindo wa twisti kwa kati ya Sh1,200 hadi 2,000 kwa kichwa kimoja lakini kulingana na maelewano kati yake na mteja.

Aidha, anasema kwamba biashara ya ususi hunawiri sana mwezi wa Disemba wakati wengi husafiri huku wengine wakija Mombasa kwa likizo.

Kulingana na Molel, kipindi hicho anaweza kuwasonga zaidi ya wateja wannne ama hata watano kulingana na kasi aliyo nayo siku hiyo.

Kuna twisti fupi ambayo huchukua takribani masaa matatu hadi manne wakati twisti ndefu huchukua kati ya masaa manne hadi matano.

Anafichua kwamba wateja wake hutoka umbali wa maeneo ya Mtwapa kaunti ya Kilifi, Mazeras, Changamwe, Likoni, Kisauni na hata Nyali.

Je, ni kwa nini akina mama wengi na hata wasichana hupenda sana kusongwa nywele na wanaume hawa kutoka jamii ya kimaasai?

Jesinta Wamboi ambaye ni mzaliwa wa Mpeketoni, Lamu anaiambia Akilimali kwamba anapenda sana kusongwa nywele na wanaume hawa kutoka jamii ya Maasai kutokana na umakini na wepesi wao wa kutekeleza kazi hii.

“Wanamakinika hadi dakika za mwisho wanapotekeleza kazi hii na wako na mwendo wa kazi sana na ikizidi ni weledi kwa kazi hii,” asema Wamboi.

Hata hivyo, Molel asema kwamba licha ya kazi ya ususi kuwa na hela kibao, kuna wakati wanakosa wateja na kulazimika kwenda nyumbani bila lolote. Anawashauri vijana kutambua vipawa vyao mapema na kujitolea mhanga kuvikuza ili kuweza kufaidi navyo mapema.

“Kutokana na ukosefu wa kazi kwa sasa vijana wanafaa kuwa wabunifu na kujituma kila mara kufaulu katika maisha,” asema Molel.

You can share this post!

KIU YA UFANISI: Kwa mtaji wa kuku wa Sh10,000 hujipatia...

Ruto kimya Mariga akihangaika

adminleo