Michezo

Warembo wa Trans Nzoia, Thika na Mathare kusaka ushindi wikendi

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye kwenye kampeni za Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) huku Trans Nzoia Falcons, Thika Queens na Mathare United Women (MUW FC) kila moja ikitafuta pointi sita muhimu.

Jumamosi hii Thika Queens itakuwa katika ardhi ya nyumbani Thika Stadium, mjini humo kukaribisha Trans Nzoia Falcons kisha Jumapili itakuwa ugenini Ruiru Stadium mjini humo kucheza na wenyeji wao Zetech Ladies (Soccer Queens).

”Bila shaka tunatarajia kibarua kigumu mbele ya Trans Nzoia Falcons,” bosi wa Thika, Fredrick Chege alisema na kuongeza kuwa wachezaji wake watajitahidi kiume kwenye jitihada za kupigania alama zote muhimu.

Thika Queens ambayo ni malkia wa zamani wa ngarambe hiyo imeonyesha dalili za kuzinduka baada ya kuanza kufanya kweli kwenye mechi za mkumbo wa pili. Licha ya kutoka nguvu sawa magoli 3-3 na Oserian Ladies wiki iliyopita inashikilia nafasi ya nne kwa alama 50.

Wasichana wa Trans Nzoia Falcons Jumapili hii watashuka katika uwanja wa Camp Toyoyo Jericho kucheza na Makolanders kwenye mchezo unaotarajiwa kuzua ushindani wa kufa mtu.

Trans Nzoia Falcons inazidi kuwasha moto mkali kwenye kampeni za muhula huu ambapo imefaulu kukamata nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 55 baada ya kucheza mechi 21. Nayo Gaspo Women inayoshikilia uongozi wa kipute hicho kwa alama 60 imepangwa kukutanishwa na Mathare United Women (MUW FC) Jumamosi hii.