• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Eti Sterling sasa haiba ya Messi, Ronaldo

Eti Sterling sasa haiba ya Messi, Ronaldo

Na MASHIRIKA

MCHANA-NYAVU katili Raheem Sterling yuko katika kiwango sawa kimchezo na magunge Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, nyota wa zamani wa Manchester City na Uingereza Trevor Sinclair amedai.

Messi (Barcelona & Argentina) na Ronaldo (Juventus & Ureno) wametawala sana mijadala ya mwanasoka bora duniani kwa zaidi ya mwongo wakijivunia taaluma zitakazokumbukwa na wapenzi wengi si tu wa soka, bali pia michezo.

Hata hivyo, Sinclair aliambia tovuti ya talkSPORT kuwa anaamini Sterling, ambaye ni mshambuliaji wa City, yuko katika ligi moja na masupastaa hao na bei yake sokoni wakati huu inafaa kuwa Sh25.5 bilioni. Anaamini pia kuwa huenda Sterling akaibuka mchezaji shapavu Uingereza imewahi kuwa nayo katika historia yake.

Licha ya kukosolewa kwa muda mrefu ikiwemo alipogura Liverpool na kujiunga na City kwa Sh6.3 bilioni mwaka 2015 na pia wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2018, Sterling ameendelea kunyamazisha wakosoaji wake kutokana na fomu yake nzuri katika ushambuliaji kwa miaka kadha sasa.

Takwimu zake ni ushahidi tosha na hakuna tashwishi kuwa amejitokeza kuwa mchezaji muhimu kwa City na nchi yake ya Uingereza. Na, baada ya kumtazama akiongoza Uingereza kuchabanga Bulgaria 4-0 na Kosovo 5-3 katika mechi alizochangia mabao mawili na pasi tatu zilizozaa magoli, Sinclair anaamini mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 24 yumo mbioni kuwa mchezaji bora duniani.

Mchezaji aliye bora

Akizungumza na tovuti hiyo mnamo Jumatano, alisema, “Raheem Sterling yuko juu kabisa, kivyangu. Bei yake sasa hivi kama si Sh25.5 bilioni, nitashangaa.

“Yeye ndiye mchezaji bora wakati huu anayechezea Uingereza na pia hutiwa wa kwanza katika orodha ya wachezaji anaotumia Pep Guardiola.

“Swali kubwa sasa ni unamweka wapi ukimlinganisha na wachezaji kama Messi na Ronaldo? Mimi namweka bega kwa bega na wawili hao. Yeye yuko katika kiwango hicho.

“Tofauti ni moja tu na ambayo hana uwezo wa kufanya chochote kuihusu, ambayo ni muda. Messi na Ronaldo wamekuwa waking’ara na bado wanazidi kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka 15 sasa na yeye ndio ameanza tu.

“Hata hivyo, akiendeleza fomu hii, watu wataanza kumzungumzia kama mchezaji bora duniani na nadhani anastahili heshima hizo.

“Ukitazama wachezaji wengine ambao wana mapato makubwa halafu uangalie wanacholeta mezani, mabao, pasi walizomega zikazalisha bao, jinsi wanavyoendesha maisha yao nje ya uwanja, yeye yuko katika kiwango kimoja na wachezaji bora duniani.

“Nilimtazama Jumamosi na alikuwa akitembea sana uwanjani na kuhifadhi nguvu jinsi anavyofanya Messi akiwa Barcelona kila wiki, na kisha anapata uhai anapoona shambulio linapoanza kukuwa na anachangamka vilivyo.

“Matokeo na uamuzi wake pamoja na mchango anaoleta katika timu ya Uingereza na City haujakuwa ukipungua kwa hivyo anafaa kuchukuliwa kama mmoja wa wanasoka bora duniani.”

  • Tags

You can share this post!

Magoha aweka wazi utaratibu wa kutathmini hatua za...

Maveterani wa Man City wala sare gozi la Kompany

adminleo