Timu ya Davis Cup ya Kenya kupandishwa daraja ikipiga Msumbiji nusu-fainali
Na GEOFFREY ANENE
KENYA italimana na Msumbiji nayo Tunisia ivaane na Madagascar kwenye mashindano ya tenisi ya Davis Cup ya daraja ya tatu ya Afrika kuamua washindi watakaoingia daraja ya pili ya Bara Ulaya/Afrika mwaka 2020.
Hii ni baada ya wenyeji Kenya kushinda mechi zao zote za Kundi B uwanjani Nairobi Club jijini Nairobi baada ya kuchapa Benin 2-1 katika mechi ya mwisho Ijumaa.
Vijana wa kocha Rosemary Owino walitwanga Benin 2-1 na kushinda kundi lake. Kenya ilianza vibaya mechi hii baada ya Albert Njogu kubwagwa na Delmas N’Tcha 6-3, 6-2. Hata hivyo, ilisawazisha 1-1 baada ya Kevin Cheruiyot kunyamazisha Sylvestre Monnou 6-3, 7-6(3). Ismael Changawa na Ibrahim Kibet walitamba katika mechi ya kuamua mshindi ya wachezaji wawili kwa wawili pale walipozidia Alexis Klegou na Amaud Sewanou 7-5, 7-6(8).
Wakenya walikuwa wamelemea Madagascar 2-1 na Algeria 2-1 katika mechi zao mbili za kwanza zilizosakatwa Septemba 11 na Septemba 12, mtawalia. Madagascar ilifuzu kushiriki mechi za nusu-fainali kama nambari mbili kutoka Kundi B baada ya kuduwaza Algeria na Benin.
Tunisia ilishinda mechi zake zote za Kundi A dhidi ya Nigeria, Msumbiji na Namibia.
Namibia italimana na Benin nayo Algeria ipepetane na Nigeria katika mechi ambazo washindi wataepuka kuangukiwa na shoka. Watakaopoteza katika mechi hizi mbili watashushwa ngazi hadi daraja la nne.
Washindi wa mechi hizo za nusu-fainali watajikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya daraja ya pili mwaka 2020, ambayo hukutanisha mataifa ya Afrika na bara Ulaya.