Raila ametuzuia kufikia Rais – wabunge
Na SAMUEL BAYA
WANASIASA wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais, Dkt William Ruto, sasa wanadai kwamba kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, amewazuia kabisa kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kujadili maendeleo na manifesto ya Jubilee.
Kauli yao ilijiri wiki chache baada ya Rais Kenyatta kusema amekatiza uhusiano na marafiki wanaokiuka maagizo yake, kuvunja sheria na kuhusika na ufisadi.
Wakiongea katika uwanja wa maonyesho ya Kilimo wa Nakuru Ijumaa, wanasiasa hao zaidi ya 30 walisema, inasikitisha kwamba licha ya kuwa katika chama cha Jubilee, imekuwa vigumu sana kwao kuonana na Rais Kenyatta kuendeleza ajenda za chama kwa manufaa ya Wakenya.
Walisema haya yalianza baada ya muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga mwaka 2018.
Mwakilishi wa akina mama wa Kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru, alisema kuwa Bw Odinga ndiye chanzo cha masaibu yao kama wabunge wa chama cha Jubilee na ambao walizoea kutangamana na Rais Kenyatta mara kwa mara.
“Kila kitu kilikuwa shwari mpaka pale Bw Raila na Rais Kenyatta walipoamua kusalimiana. Hapo mambo sasa yakaanza kwenda kombo hivi kwamba imekuwa vigumu sana kumfikia Rais kujadiliana kwa pamoja kama wana Jubilee,” akasema Bi Waruguru.
“Rais alikuwa akitusikiliza vizuri sana kama wana Jubilee na alichukulia kwa uzito kila jambo ambalo tungemuelezea wakati huo. Cha kusikitisha ni kuwa, baada ya Bw Odinga kuingia kati, kila kitu kiliharibika kabisa,” akaongeza mbunge huyo.
Hata hivyo, viongozi hao kwa kauli moja walisema Raila Odinga hatafaulu katika kuwagawanya na kwamba wataendelea na juhudi zao za kumpigia debe Naibu Rais kuwa rais 2022.
“Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto waliweka ahadi kwamba kila mmoja atahudumia Wakenya kwa vipindi viwili viwili na hivyo basi, baada ya Rais Kenyatta kumaliza muhula wake tutakayemchagua ni William Ruto. Huo ndio mkataba ambao tuliweka kama wana Jubilee na hautavunjika kamwe,” akasema Bi Kihika.
Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki, Bw David Gikaria alimlaumu Bw Odinga kwa masaibu ambayo Jubilee inapitia.
“Kuna huyu mzee ambaye kila mtu anamjua. Amechoka na hawezani tena na siasa za taifa hili. Lakini ameingia kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto. Lengo lake ni kuleta mgawanyiko ambao awali haukuwepo,” akasema Bw Gikaria.
Mbunge wa Subukia Bw Samuel Gachobe alisema kuwa mabadiliko ya katiba ambayo yanasukumwa sharti yawe ya kunufaisha mwananchi wa kawaida anayepitia hali ngumu ya kiuchumi na wala sio kuongeza mzigo tena kwa Wakenya.
Njama
Naye Bi Kihika alisisitiza kwamba, mpango wa BBI ni njama ya Bw Odinga kutaka kuingia uongozini kwa mlango wa nyuma baada ya kushindwa urais mara nne.
“Baada ya kuhisi kwamba hakuna mahali anaenda, sasa ameamua kutumia mabadiliko hayo ya katiba kuzusha vitimbi nchini. Tunafahamu msukumo wake wa kutaka katiba ifanyiwe marekebisho ili atue uongozini lakini hilo tumeliona na maamuzi tumefanya,” akasema Bi Kihika.
Naye mwakilishi wa akina mama katika kaunti ya Uasin Gishu Bi Gladys Shollei alisema mpango wa BBI hauna mashiko kwa sababu kuna utulivu wa kutosha nchini.
“Zile salamu za kweli zilikuwa ni 2013 wakati vyama vya TNA na URP vilivunjwa na kukaanzishwa chama kimoja cha Jubilee.
Kulingana na mkataba wa wakati huo, baada ya Rais Kenyatta kutawala kwa miaka 10, sasa ingekuwa zamu ya naibu Rais William Ruto kuchukua uongozi. Huo ndio msimamo ambao uko na haujabadilika,” akasema Bi Sholei.