Binti kiungo wa Lionesses anavyonoa makali yake
NA RICHARD MAOSI
Mchezo wa raga unaendelea kupata umaarufu mkubwa kote nchini kutokana na ufuasi mkubwa wa mashabiki, wanaondelea kuushabikia kila kukicha
Kinyume na matarajio sio wengi wanaofahamu kuwa pia kuna timu za akina dada zinazoshiriki katika aina hii ya michuano ya kipekee,inayohitaji maguvu na ujuzi kupita kiasi.
Labda ni kwa sababu ya mazoezi mazito ambayo huwafanya baadhi ya akina dada kutoweza kustahimili shinikizo lake, ikiaminika kuwa mshiriki ni lazima awe katika hali nzuri ya afya.
Mazoezi yao mengi yakiwa ni yale ya kututumua misuli na kunyoosha viungo kabla ya kushiriki katika aina nyingine ya mazoezi ambayo tunaweza kusema ni mepesi.
Dimba la Taifa Leo lilibahatika kujumuika na mchezaji nguli wa timu ya akina dada ya taifa Kenya Lionesses, Grace Adhiambo mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya Spotlight Academy Nakuru.
Grace anasema alianza kucheza raga akiwa kwenye shule ya msingi ya Freehold inayopatikana katika mtaa wa Kenlands, kilomita 3 hivi kutoka mjini Nakuru.
Anasema kufikia sasa kikosi cha timu ya akina dada cha raga kinashikilia nambari 28 kote ulimwenguni, baada ya kukwea jedwali kutokana na jumula ya matokeo mazuri wanayoandikisha kila wakati.
Akiwa ndiye mchezaji wa kipekee kutoka eneo la Bonde la ufa anasema, mwalimu wake George Otieno alimsaidia kupata hamasa mbali na kumsaidia kushiriki michuano ya kirafiki.
Grace anasema amekuwa akifanya mazoezi yake mara mbili kila wiki,ili kujiongezea tajriba na uwezo wa kukabili shinikizo la michuano ya raga inayohitaji weledi wa aina yake.
Aidha akiwa shuleni hupasha misuli yake moto katika uwanja wa Mazembe na wakati mwingine Nakuru Athletics Club (NAC),ngome ambayo imezalisha talanta za haiba kubwa katika ulingo wa spoti.
Grace anasema kuwa inagwa serikali kuu haijawekeza kikamilifu katika mchezo wa raga hasa kwa timu za akina dada, matumaini yake ni kuja kuwa mchezaji wa kimataifa siku moja katika rubaa za kimataifa.
Anasema ni ndoto ya kila mchezaji mwenye bidii kuja kuwajibikia timu ya taifa katika kiwango chochote cha mashindano,ima ni ya ligi au ukanda wa bara.
Grace anasema kuwa kupitia spoti amefanikiwa kutembelea mataifa mengi ndani na nje ya bara Afrika, ikizingatiwa kuwa yeye ni miongoni mwa wachezaji wachanga katika timu ya taifa ya akina dada.
Timu ya Kenya Lionesses ambayo mwaka uliopita ilinyakuwa taji la akina dada barani Afrika baada ya kulemaza Uganda katika fainali 29-7 nchini Botswana.
Lionesses imekuwa ikiwakilisha taifa katika michuano ya kitaifa na kimataifa kwa wachezaji 7 na 15 kila upande,wachezaji chipukizi wakiibukia kujaza pengo ya wale waliobobea.
Mwaka uliopita wakiandikisha matokeo mema katika historia ya raga ya akina dada kuwahi kutokea nchini,ambapo katika michuano ya jumuia ya madola walifika fainali na kuridhika na nambari tano kwa jumla.
Timu nyingi kutoka Urusi,Uchina Uingereza na Uholanzi zikionekana kuwania huduma zake hasa hasa tangu ajipatie nafasi katika kikosi cha kwanza kwenye timu ya taifa.
Anasema mkufunzi wa timu ya taifa Kenya Lionnesses Felix Ade Oloo aliona uwezo wake ndipo akampendekeza kujaza nafasi ya kikosi cha kwanza.
Inagwa alipata changamoto kubwa kukabiliana na wachezaji wenye uzoefu mkubwa hatimaye juhudi zake zilizaa matunda,baada ya kuonyesha ukakamavu na wala hakukata tamaa.
Anaamini kuwa timu ya raga ya akina dada nchini itakuja kufika mbali na hata ina uwezo wa kunyakua kombe la dunia.
Ujumbe wake kwa wazazi anawashauri kuwaruhusu watoto wao kutumia talanta zao ili waje kujiendeleza kimaisha.
Grace anaamini kuwa ingawa masomo ni muhimu,michezo pia ni muhimu zaidi kwani ni chombo cha kuwaunganisha watu kutoka matabaka na mataifa mbalimbali duniani.
“Sawa na masomo kipaji cha kucheza vilevile kinaweza kumfikisha mtu mbali na hata kaja kuwa mtu wa kutajika duniani kama vile Christiano Ronaldo anatambulika kwa sababu ya michezo,”akasema.