• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Wagura ufugaji wa ng’ombe, wageukia mbuzi wa maziwa

Wagura ufugaji wa ng’ombe, wageukia mbuzi wa maziwa

NA RICHARD MAOSI

Kaunti ndogo ya Rongai inayopatikana viungani mwa mji wa Nakuru ni eneo linalopokea mvua kidogo kila mwaka, jambo linalowapatia wakulima wengi changamoto wakati wa kutafutia mifugo wao chakula na maji.

Wakulima wengi hapa ni wafugaji wa ng’ombe na pia hukuza mimea kama vile mahindi ,maharagwe,parachichi na matikiti maji,ila miaka ya hivi karibuni mabadiliko ya hali ya anga yamefanya wao kutalii nyanja nyingine ya ukulima.

Mmoja wao ni Patrick Ndung’u Chege anayewafuga mbuzi wa maziwa badala ya ng’ombe wa kawaida, akisema kuwa gharama yake ni nafuu, na ni kilimo kinachoweza kumpatia mkulima tija .

Tulimkuta katika kipande chake cha ardhi akiendelea kuwakama mbuzi wake,kabla ya kusafirisha maziwa yake sokoni ambayo anasema yanawaniwa na wanunuzi kutoka maeneo yanayozunguka Nakuru.

Aidha anasema kilichomsukuma kuanzisha mradi huu ni hitaji la kujiongezea kipato,mbali na kushirikiana na wakulima wengine wenye nia ya kujiinua kimapato kutoka Rongai.

Patrick Ndungu anasema mbuzi wanahitaji majani yaliyokaushwa kwani huwa na kiwango cha juu cha virutubishi. Picha/ Richard Maosi

Patrick anasema kwa siku moja anaweza kupata lita nane ya maziwa kutoka kwa mbuzi watatu,ambapo lita moja sokoni huuzwa kwa 125,mara tatu bei ya maziwa kutoka kwa ng’ombe.

Hii inamaanisha kuwa kwa wiki moja anaweza kutengeneza baina ya 7,000-8,000 kutoka kwa mbuzi watatu,ambapo humtengenezea zaidi ya 30,000 kwa mwezi ikizingatiwa kuwa yeye pia ni mkulima wa mahindi.

Kipato hiki kimemsaidia kuwasomesha watoto na kujinunulia kipande cha ardhi,na malengo yake ni kupanua uwanda wa ufugaji kwa sababu baada ya muda mfupi amekubali mbuzi ni bora kuliko ng’ombe.

“Haja yangu kubwa kuanzisha mradi huu ni kupatia familia yangu maziwa ya hali ya juu,lakini sasa mradi wenyewe umekuwa ni kitega uchumi,” Patrick akasema.

Kwa mtaji kidogo alianza na mbuzi mmoja,kisha wakazaana na sasa anafuga spishi mbalimbali ambazo ni saanen na Alpine ambao huvumilia hali ngumu ya mazingira na pia wamezowea kula kiwango kidogo cha majani yanayoweza kupatikana.

Mazingira safi na lishe bora ni baadhi ya mambo ambayo mkulima anastahili kuzingatia kabla ya kujitosa katika ufugaji wa mbuzi wa maziwa. Picha/Richard Maosi.

Lakini hata hivyo Patrick anasema kuna baadhi ya mambo ambayo mkulima anapaswa kuzingatia wakati wa kufuga mbuzi wake,kwanza ahakikishe kuwa kibanda cha mbuzi kimeinuliwa kidogo kutoka ardhini mita mbili hivi ili kuhakikisha kuwa viroboto na kupe hawayashambulii makazi yao.

Anasema hii itapunguza gharama ya kuwatibu kwa kupulizia dawa mara kwa mara , jambo ambalo linaweza kuzuilika kutokana na ukulima sahihi wa kuwatunza mbuzi katika mazingira bora tena safi.

Patrick huwakamua mbuzi watatu kila siku, na anaweza kupata lita nane au zaidi,jambo linalomfanya kuungama kuwa amejitengenezea nafasi ya ajira badala ya kutegemea vibarua huko nje visivyoweza kutabirika.

Anawashauri wakulima kujikita katika kilimo biashara ili waweze kupata soko kwa bidhaa zao wanazozalisha kwa wanunuzi.Anasema katika mataifa yaliyoendelea ukulima wa mbuzi umeleta viwanda vingi vinavyojihusisha na maziwa ya mbuzi.

Patrick Ndungu akiwatunza mbuzi wake wakati Akilimali ilipomzuru katika kaunti ndogo ya Rongai eneo la Nakuru majuzi. Picha/Richard Maosi

“Hiki ni kilimo kinachoweza kuendeshwa na watu wanaomiliki mashamba na wale wasiokuwa na mashamba mijini,muradi waelewe kanuni zinazohitajika kustawisha mradi wenyewe,”akasema.

Mbuzi anahitaji nafasi ndogo wakati wa kumfuga ambayo ni mita nne mraba(4 by 4) na wala hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kulalamika kuwa haweza kupata nafasi kama hiyo, kuendeshea mradi wake.

Miongoni mwa mbuzi wake kuna wale wanaokamuliwa,wengine ni wajawazito na kuna mbuzi wadogo waliozaliwa hivi karibuni ili kuendeleza kizazi cha mifugo hawa.

Aidha mbuzi wanaweza kutumia majani ya kawaida kama vile magugu na miche,pia wao huywa kiwango kidogo cha maji,wala hawahitaji matibabu ya kila wakati,tukizi ambalo ni nadra sana kuwakumba.

“Katika maeneo ambayo maziwa ya mbuzi yamekuwa yakitegemewa wengi wanaoyahitaji huyatumia kwa sababu za kiafya na bei yake huwa kati ya 100-200 kwa lita,”akasema Bw Patrick.

Ambapo kimatibabu watoto wanaokuwa na udhaifu wa kimwili na matatizo ya kusimama au kutembea wanashauriwa kuyatumia maziwa haya, ambayo huwa na virutubishi muhimu vya calcium,magnesium na patassium.

Vilevile maziwa ya mbuzi husaidia watoto kukua haraka na kuwapatia uwezo wa kukomaa ubongo mapema ili wasipate changamoto wakati wa kuzungumza.

Patrick anasema amefaidika na ufugaji wa mbuzi kwa sababu anapatikana karibu na mji wa Nakuru na Eldoret,anasema wakulima wengi huanzisha mradi wenyewe bila kufahamu soko lake.

Hata hivyo anahimiza kuwa mbuzi aliyejifungua anastahili kupatiwa chakula kizuri wakati akinyonyesha vitoto,chakula hiki kinastahili kubadilishwa wakati wote,ambapo virutubishi katika chakula viongezewe kati ya mwezi mmoja au miwili.

Vitoto vya mbuzi wanastahili kuachishwa kunyonya baada ya miezi mitatu bila kutegemea aina nyingine ya lishe,watoto wa kiume wapatiwe maziwa mengi kuliko wale wa kike.

Mbuzi wa maziwa wanastahili kufugiwa katika eneo la Zero Grazing ili wasizurure wakitafuta chakula,pia wawekewe sehemu safi ya kulala ili wasije wakakanyaga lishe zao kuzuia mkurupuko wa maradhi.

“Mbuzi hupendelea kula urefu wa magoti na pia katika sehemu ya kulala mbuzi wanapenda kulala juu na hawawezi kubali kulala chini,sakafu inahitaji kutandaziwa mbao,chumba hiki kigawanywe kwa sehemu mbili sehemu moja ikiwa ni ya kulala,”aliongezea Bw Patrick.

Kwa kawaida mbuzi wachanganyiwe chakula kama vile hay,mwarobaine na mbogamboga ambapo mkulima ahakikishe kuwa mboga zake hazina majimaji.

Alisema majani yaliyokaushwa ni chakula bora kinachohitajika kulisha mboga kwa sababu hutoa madini ya hali ya juu.Ikumbukwe kuwa mbuzi wanafaa kuongezewa sukari guru katika lishe au maji yao ili wafurahie chakula chao na maji.

Patrick anasema dalili za mbuzi kuwa mgonjwa ni kukosa hamu ya chakula ,kuregea na ngozi yake kuchakaa.Pia Patrick anasema vikundi vinaweza kuungana na kununua mbuzi walioboreshwa na kuanzisha mradi kama jamii.

Bidhaa zinazotokana na mbuzi kama vile ghee na Cheese ni bei ghali na wala hazina mfano wake ijapo katika thamani yake.

Patrick anatoa wosia kwa wizara husika ya kilimo kuwakumbuka wakulima wa mbuzi na kuwekeza katika ufugaji wa kilimo ili kuwapatia wakulima mashauri ya mara kwa mara.

You can share this post!

Kipa ngome ya kuaminika michumani Mount Kenya University FC

RISSEA: Kituo kinachohifadhi utamaduni wa jamii za Pwani

adminleo