Hatua za kuboresha ufugaji wa ng'ombe wa maziwa
NA RICHARD MAOSI
Karibu na kaunti ya Baringo eneo la Eldama Ravine kuna kiwanda cha maziwa kinachowasaidia vijana kupata nafasi ya ajira, kutokana na uandaaji wa bidhaa zinazotokana na maziwa kama vile maziwa mala.
Kiwanda cha Sabatia kilianzishwa na wakoloni lakini kimefanikiwa kukabiliana na mawimbi ya soko, na hivi sasa kinatumika kutoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana wanaokaa katika kaunti ya Baringo na viungani mwake.
Kuanzia 1963 wageni walianzisha kiwanda hiki ili wakulima wengi kutoka eneo hili ambao ni wafugaji wapate soko kwa maziwa yao.
Hivi sasa kazi yake kubwa ni kukusanya maziwa,kuyahifadhi katika vyombo maalum vya kisasa na kutafuta soko ndani na nje ya kaunti ya Baringo.
Awali kiwanda chenyewe kilianza na wakulima 658 lakini kufikia sasa idadi yao imeongezeka na kufikisha tarakimu ya zaidi ya 3000.Hii ikionyesha kuwa wamepiga hatua kubwa isiyokuwa na kifani.
Akizungumza na Akilimali Bi Rose Maiyo meneja anayesimamia shughuli katika kiwanda hicho, anasema kuwa hili ni eneo ambalo lilikuwa ni makazi ya wakoloni lakini juhudi za wakulima ziligeuza sehemu yenyewe kuwaongezea kipato.
“Wazungu waliporejea makwao waliuza shamba hili kwa wenyeji kwa mkopo,ambao ulistahili kulipwa baada ya kipindi Fulani,”akasema Bi Maiyo.
Hata hivyo alielezea kuwa mafanikio katika ukulima wa ngómbe wa maziwa yanategemea mambo matano tu ,ili mkulima aweze kupata tija na manufaa ya muda mrefu.
- Upatikanaji wa malisho na mazingira ya ufugaji
Anashauri kuwa kabla ya mkulima yeyote kuingilia maswala ya ufugaji wa ngómbe, ni lazima awe na maarifa ya kutosha namna ya kuwalisha mifugo wake katika mazingira mwafaka.
Mazingira hayo sio lazima yawe na malisho lakini anaweza kutumia raslimali haba zinazopatikana,kwa ufaafu wa mifugo wake na soko la maziwa kwa ujumla.
Bi Maiyo anasema malisho mwafaka husaidia ng’ombe kuzuia uwezekano wa mkurupuko wa maradhi kwa mfano kititi(mastitis), na vilevile kuboresha hadhi ya maziwa kwa wanunuzi.
Lishe hizi zinastahili kuchanganywa na zile za viwandani, ili mifugo wapate aina mbalimbali ya malaji bila kutegemea nyasi za kawaida zisizokuwa na virutubishi vya kutosha.
Ni kwa sababu hiyo wakulima waliamua kuungana kutoka kaunti ya Baringo na eneo la Eldama Ravine, na kuanzisha kiwanda cha maziwa ili watengeneze hela ambazo zingewasaidia kulipia mkopo.
Maiyo alifichulia akilimali kuwa kiwanda chenyewe kinapatikana katika sehemu bora kufanyia bishara,kwani ni eneo ambalo linapakana na barabara hivyo basi ni rahisi kwa wakulima kusafirisha maziwa yao kutoka mashambani hadi katika kiwanda.
Pili alisema kuwa mazingira yanapakana na wakulima wengi wanaotekeleza kilimo cha ufugaji wa ngómbe jambo linalofanya maziwa kupatikana kwa urahisi.
Ingawa wakati mwingine ukame husababisha changamoto za kupata lishe, kwa wakulima wanakabiliana na changamoto hizi kwa kuwashauri wakulima namna ya kupatia mifugo wao lishe zinazostahili mara tatu kwa siku.
Kiwanda cha Sabatia kimekuwa katika mstari wa mbele kutoa utaratibu kwa wakulima wanaokuza lishe ya mifugo kwa kuwahimiza wajaribu lishe nyingine kama vile hay ambazo hukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.
2. Wakulima wasaidiwa kupata mikopo na huduma za matibabu.
Kulingana na Bi Maiyo changamoto kubwa zinazowakumba wakulima siku hizi ni mikopo ya kujiendeleza , kama vile hela za kutengenezea mifugo sehemu kwafaka ya kukaa.
Anaona kuwa endapo washikadau watajitokeza kuhakikisha wakulima wanapata hela za kutosha,watafanikiwa kuboresha kilimo hiki na kuwainua wakulima wengi kutoka mashinani.
Aidha huduma za kitaaluma zitahitajika ili kumsaidia mkulima aweze kukabiliana na mkurupuko wa maradhi mbalimbali,yanayoweza kusababishwa na kupe kwa kununua dawa za kupulizia.
“Kwa mfano wakulima wetu wanaweza kupata madawa pamoja na lishe kutoka kwenye duka letu la kijumla kisha wakalipia polepole baadae pasipokuwa na riba kubwa,”akasema.
Tunawasaidia kutibu mifugo wao na pia kuandaa makongamano ya mara kwa mara yanayolenga kuwaleta wakulima pamoja kubadilishana mawazo.
Maiyo aliongezea kuwa huduma hizi zimekuwa zikipiga jeki mapato ya kiwanda ambapo wanaweza kutengeneza hadi milioni 96 kila mwaka.
3. Kuhakikisha mifugo wako katika hali ya utulivu ili kupata bidhaa safi
Bi Maiyo anasema kuwa endapo afya ya mifugo na lishe itazingatiwa,mkulima hana budi kupata mavuno kutokana na bidii zake.Mifugo wasipokuwa katika hali ya utulivu wanaweza kupunguza kiwango cha maziwa.
Aliongezea kuwa mifugo wanaweza kufugwa mbali na mji,ili kupunguza usumbufu wa kelele kutoka kwa magari na moshi wa viwandani unaowachefua ngómbe wa maziwa kwa urahisi.
Anasema ili kudhibiti maharamia wanaopatikana sokoni ni vyema viwanda kuchukua maziwa yaliyokaguliwa vya kutosha, ili kuhakikisha kuwa hakuna vimelea.Maziwa safi ni yaleyaliyokamwa bila kumshurutisha ngómbe.
Kwa upande mmoja anaona kuwa sio jambo la busara kupulizia mifugo wako dawa kila wakatii kwani huenda ikaharibu ubora wa maziwa.
Pia anawasuta baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakiongezea maziwa yao maji kwani huua soko, na kuletea viwanda hasara lakini teknolojia imesaidia kupima na kubaini kiwango cha maji kinachoweza kupatikana ndani ya maziwa.
4. Kuongezea maziwa thamani
Mbali na kujikita kwenye ukulima wa maziwa ili mkulima aweze kujiongezea kipato,kiwanda kinaweza kutengeneza bidhaa nyinginezo zinazotokana na maziwa kama vile yoghurt,cheese na ghee.
Anasema kuwa huduma kama hizi zitamwongezea mkulima mapato zaidi ya mara mbili kwani huduma zote zinazohusiana na uongezaji wa thamani, katika maziwa hupandisha thamani yake.
“Kwa mfano lita moja ya yoghurt inaweza kutoka hadi 150 ,ikiwa hii ni zaidi ya mara tatu bei ya kawaida ya maziwa,”aliongezea.
“Thamani ya maziwa huongezeka endapo yatahifadhiwa vyema katika vyombo maalum,”akasema.
5. Kukumbatia teknolojia mpya za ukulima.
Bi Maiyo anaamini kuwa teknolojia imekuja na faida nyingi kuliko hasara,teknolojia nafuu na za kuimarisha mapato ni jambo la kimsingi kwa mkulima yeyote.
Anawashauri wakulima kukumbatia teknolojia mpya za kilimo kama vile majokofu yanayoweza kuhifadhi kiwango kikubwa cha maziwa kwa muda mrefu.
Anasema wanaweza kutumia trekta kulima vipande vyao vya ardhi, na kupanda lishe za kisasa kama vile hay ,ambapo pidi zinapovunwa zinaweza kuongezewa virutubishi muhimu.