Bandari wamiminiwa sifa tele baada ya kutandika Watunisia
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
USHINDI wa Bandari FC katika mechi yao ya raundi ya kwanza mkondo wa kwanza ya Kombe la Mashirikisho la Afrika kwa mabao 2-0 dhidi ya US Ben Guerdane ya Tunisia umepongezwa na wadau wa soka Pwani.
Mwanachama mpya wa bodi ya klabu hiyo, Twaha Mbarak aliutaja ushindi huo wa Jumamosi uwanjani Kasarani kuwa fahari kubwa mkoani humu na akawa na matumaini makubwa timu hiyo itafanya vizuri mechi ya marudiano.
“Huu ni ushindi ambao utabakia kuwa wa kihistoria kwani timu nyingine ya Pwani iliyowahi kushiriki mashindano haya, Lake Warriors, miaka ya 1980, ilibanduliwa mapema,” alisema afisa huyo mpya wa Bandari FC.
Mbarak aliwapongeza wachezaji, maafisa wa benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na kuifanya Bandari kuwa mojawapo ya timu kubwa inayotambulika kote Afrika Mashariki.
“Ushindi huo ni kielelezo kizuri cha kuifanya Bandari iangaziwe sio Afrika Mashariki pekee, bali barani Afrika kwa sababu Watunisia wanatambulika kuwa na soka ya hali ya juu. Ninaamini vijana wetu watafanya vizuri zaidi watakapocheza ugenini,” alisema Mbarak.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally aliipongeza Bandari kwa ushindi wao huo na kueleza kuwa hana shaka timu hiyo itashiriki raundi ijayo.