• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:40 AM
KINA CHA FIKIRA: Tuwanie kuunda Baraza la Kiswahili wala si la Lugha

KINA CHA FIKIRA: Tuwanie kuunda Baraza la Kiswahili wala si la Lugha

Na KEN WALIBORA

WIKI iliyopita Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita)—Tanzania, lilinialika kushiriki tamasha za Kiswahili na Utamaduni katika viunga vya mji wa Arusha mahali paitwapo Usa-River.

Kwa siku tano nilikuwa Usa-River kwa ajili ya tamasha hizo za Kiswahili na Utamaduni.

Kama zilivyo hafla nyingi za Kiswahili, muhimu si kuwapo kwa halaiki ya watu, bali mazingira ya kirafiki na udugu na ucheshi.

Kulikuwa na washereheshaji wa namna yake; watatu kwa jumla, wakiongozwa na Bi Kawthar na Bw Sovu. Ila ninachotaka kusema ni kwamba nilifarijika sana kuona washerehereshaji wenye weledi wa kupigiwa mfano, wanaosema Kiswahili kwa mazoea na kujiamini na wanaocheka huku wanakosoa na kukosolewa.

Nimehudhuria hafla nyingi katika maisha yangu, ila sijawahi kufarijika kama nilivyofarijika katika hili kongomano la Arusha.

Fikiria kwa mfano Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe, kadhuhuria tamasha kwa siku mbili mfululizo. Ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi na akaganda habanduki kama washiriki wanyonge kama mimi.

Ajabu ni kwamba hata nilikuwa mwenyekiti wa kikao kimoja na kukosa kuona waziri akiinua mkono wake kutaka kuchangia, sikuitiwa polisi kuninasa. Unyenyekevu kama huo sijapata kuuona.

Jambo jingine zuri lililotokea ni kwamba Baraza la Kiswahili la Taifa-(BAKITA) lilizindua rasmi kanuni zake za utendaji. Baraza hili limekuwa chombo cha kushauri kuhusu maendeleo na matumizi ya Kiswahili Tanzania Bara kwa vile Zanzibar wana chombo chao kiitwacho BAKIZA na mwenyekiti wake Mohamed Khatibu alikuwapo kwenye tamasha.

Ilikuwa furaha iliyoje nikiwa Usa-River, Arusha kusikia kwamba kuundwa Baraza la Kiswahili Kenya kulikuwa karibu kutimia?

Najua fika kwamba wafurukutwa kama vile Kimani Njogu, Clara Momanyi, Fred Ojienda, Mohamed Abdulaaziz wamekuwa kwenye mstari wa mbele kulipigania jambo hili hata kabla ya kupitishwa kwa Katiba ya 2010.

Hata mimi mnyonge wenu nimekuwa nimo katika harakati hizo na tumekaa vikao visivyokuwa na hesabu kujaribu kuishawishi serikali itimize ndoto hii.

Ilmradi nilifarijika sana kusikia nikiwa Tanzania kuhusu hatua zinazopigwa kuliafikia hili. Kuna mengi Kenya inaweza kujifunza kutoka Tanzania.

Iwapo Kenya itaunda Baraza la Kiswahili, haina budi kulipa makali ili lisiwe mbwa asiyekuwa na meno au tembo asiyekuwa na pembe. Itabidi Kenya itunge kanuni za baraza zitakazohusisha utendaji wa wadau wote, hasa vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili kama wenzo wa kujielezea.

Ninashauri Kenya iunde Baraza la Kiswahili wala si Baraza la Lugha.

La kuepuka kutoka Tanzania ni kuwa na mabaraza mawili ya lugha; BAKIZA na BAKITA. Tunajenga nyumba moja tusipiganie fito.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Mbinu za upanuzi wa leksikoni katika...

MAPITIO YA TUNGO: ‘Naomba Unisamehe’ ni novela...

adminleo