• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
MSHAIRI WETU: Antony Nyaga almaarufu ‘Hakuna Matata’

MSHAIRI WETU: Antony Nyaga almaarufu ‘Hakuna Matata’

Na CHRIS ADUNGO

USHAIRI ni sanaa ambayo hutumiwa kumulika jamii.

Mtu hawezi kabisa kubobea katika sanaa hii iwapo hana uwezo wa kuhimili mapigo ya kukosolewa na washairi stadi zaidi yake. Kuwa mshairi shupavu kwahitaji mtunzi ajifunze kutoka kwa wengine na kuwa radhi kupokea maelekezo ya watangulizi wake.

Haya ni maoni ya mshairi Antony Nyaga almaarufu ‘Hakuna Matata’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa Aprili 24, 1996, katika eneo la Ishiara, Kaunti ya Embu katika familia ya Bi Rose Igoki na Bw Alvan Nyaga.

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya Mbaraga, Ishiara Embu ambako nilifanyia mtihani wa KCPE mnamo 2010 na kujiunga na Shule ya Upili ya Kanyuambora, Embu mnamo 2011 hadi nilipofanya mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2014. Baadaye 2015, nilijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo kwa sasa nasomea Shahada ya Ualimu (Kiswahili na Dini) kwa matarajio ya kufuzu mnamo Disemba mwaka huu.

Nani na nini kilikuchochea kupenda ushairi?

Nilivutiwa sana na ushairi tangu nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Katika vitabu ‘Kiswahili Mufti’ vya Wallah Bin Wallah, kulikuwamo na mashairi mazuri na mepesi sana. Hivi ni vitabu tulivyokuwa tukivitumia madarasani. Nilipenda sana kukariri baadhi ya mashairi hayo wakati wa hafla au sherehe mbalimbali shuleni.

Nikiwa shule ya upili, aliyekuwa mwalimu wangu Bi Bessy aligundua kipaji changu na kunihimiza kukikuza baada ya kuniaminisha kuwa kingenifaidi sana katika maisha ya usoni.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Nikiwa mwanafunzi wa darasa la tano. Nililipa shairi hilo kichwa ‘Mbwa Wangu’. Mwalimu wangu wa Kiswahili wakati huo Bw Ireri Ngomora, alinipongeza sana na kuninunulia zawadi. Alinihimiza kuendelea kutunga na tangu hapo, sijarudi nyuma kwa kuwa napiga hatua kila siku.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Huangazia mambo yanayotendeka kila siku katika jamii, mfano siasa, ndoa na mapenzi na masuala mengineyo ibuka.

Unahitaji muda gani kutunga shairi moja?

Muda wa kutunga hutegemea ufupi au urefu wa shairi, ama wepesi au ugumu wa mada ninayoishughulikia. Hata hivyo, nina uwezo wa kutunga shairi la tarbia lenye beti sita hivi chini ya kipindi cha dakika 15 iwapo nitakuwa nasukumwa na hisia fulani za ndani kwa ndani.

Mbona mashairi ya arudhi?

Huimbika vizuri na kwa urahisi kwa sababu huwa na mapigo ya sauti (vina) yaletayo urari na mdundo fulani wa kingoma wakati shairi linapoimbwa, kukaririwa au kughaniwa. Mbali na kuwa pia kipimo kamili cha ukomavu wa mshairi, tungo za arudhi hutufundisha umuhimu wa kuzingatia kanuni hata katika maisha ya kawaida.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Rafiki zangu wanapokuwa na shughuli mbalimbali kama vile harusi, sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa au mahafali, wao huniomba niwaandikie mashairi kwa ada fulani. Pia hutungia shule mbalimbali kwa minajili ya tamasha za muziki. Fedha nizipatazo hunisaidia kwa kiasi fulani kuyakidhi baadhi ya mahitaji ya kimsingi nikiwa chuoni.

Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na ushairi wako?

Naam! Nilituzwa katika Shule ya Upili ya All Saints Kigari, Embu nilikofanyia mafunzo ya tamrini. Niliwatungia wanafunzi wa shule hiyo shairi ambalo walitamba nalo katika mashindano ya kitaifa ya tamasha za muziki na drama.

Nikiwa mwanafunzi wa shule ya upili, nilitunga mashairi ya kughaniwa wakati wa hafla mbalimbali na aliyekuwa Mwalimu Mkuu, Bw Mutero akanituza si haba. Aidha, nimevipokea vitabu vingi kutoka kwa mhadhiri wangu Dkt Hamisi Omar Babusa kutokana na bidii zangu katika utunzi wa mashairi.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na makuzi ya ushairi?

Ninapania kuandika diwani na pia kitabu cha kufundishia ushairi katika kiwango cha shule za upili.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Huwa ninaandika Hadithi Fupi na Hadithi za Watoto ambazo natarajia zitachapishwa hivi karibuni.

Unawashauri nini washairi chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Chipukizi watie bidii na wasife moyo. Kila jambo huanza kwa hatua. Washairi wa zamani waendelee kuwashika mkono watunzi chipukizi.

You can share this post!

SEKTA YA ELIMU: Serikali iongeze ufadhili na usambazaji wa...

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimnyima asali uhusiano wetu ukaingia...

adminleo