Michezo

KPL: Bandari na Zoo Kericho kutoana jasho leo Jumatano mjini Mombasa

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KAMPENI za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) zinarejelewa leo Jumatano kwa mchuano utakaowakutanisha Bandari FC na Zoo Kericho katika uwanja wa Mbaraki Sports jijini Mombasa.

Kipute hiki ni sehemu ya mechi mbili za KPL ambazo ziliratibiwa upya wiki jana ili kuwawezesha Bandari na Gor Mahia kushiriki kikamilifu kivumbi cha kuwania ufalme wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) na Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).

Gor Mahia ambao walirejea humu nchini hapo jana baada ya chombo chao kuzamishwa kwa 4-1 na USM Alger nchini Algeria, wamepangiwa kumenyana na Chemelil Sugar hapo kesho uwanjani Moi, Kisumu.

Zoo ambao walikwepa shoka ambalo vinginevyo lingaliwateremsha daraja msimu jana, walifungua kampeni za muhula huu kwa matao ya juu kwa kuwakomoa Chemelil Sugar 3-1.

Kwa upande wao, Bandari walilazimishiwa sare tasa na Mathare United uwanjani MISC Kasarani mnamo Agosti 31.

Tangu wapandishwe daraja kushiriki kivumbi cha KPL mnamo 2017, Zoo Kericho wanajivunia kuwapiga Bandari mara moja pekee huku mechi tatu nyinginezo zilizowakutanisha zikitamatika kwa sare.

Kati ya mechi hizi zote, tatu zimekamilika kwa mabao matatu au zaidi kupachikwa wavuni huku mchuano mmoja pekee ukimalizika kwa sare tasa.

Isipokuwa mchuano wao wa wikendi iliyopita ambao uliwashuhudia Bandari wakiwapepeta US Ben Guerdane ya Tunisia, miamba hao wa soka kutoka Pwani wamesajili sare katika mechi saba zilizopita kwenye mapambano yote. Ushindi wa mwisho uliovunwa na Bandari FC ligini ni mchuano uliowashuhudia wakiwapepeta Zoo mnamo Mei 19, 2019.

Zoo watajibwaga ugani wakitarajia kuendeleza ubabe ambao umewashuhudia wakisajili ushindi mara nne, kuambulia sare tatu na kupoteza mchuano mmoja pekee kati ya mechi nane zilizopita.

Mchuano wa leo Jumatano utakuwa jukwaa mwafaka kwa kiungo Danson Chetambe wa Bandari kuchuana na waajiri wake wa zamani baada ya kuagana na Zoo mwishoni mwa msimu uliopita.

Kwa upande mwingine, Gor Mahia watakuwa wakilenga kujinyanyua na kuziwekea dira kampeni zao za KPL muhula huu baada ya matumaini ya kusonga mbele katika CAF kudidimizwa na USM Alger ugenini.

Kichapo cha 4-1 nchini Algeria kinawasaza Gor Mahia katika ulazima wa kusajili ushindi wa angalau mabao matatu bila jibu watakaporudiana na USM Alger jijini Nairobi mnamo Septemba 29.

Baada ya kuchuana na Chemelil Sugar, Gor Mahia ambao kwa sasa wananolewa na kocha Steven Pollack watapimana ubabe na wanabeki wa KCB ambao kwa sasa wanaongoza jedwali la KPL chini ya ukufunzi wa Zedekiah ‘Zico’ Otieno ambaye pia ni kocha msaidizi wa Harambee Stars. Mechi kati ya Gor Mahia na KCB itapigiwa ugani Kenyatta, Machakos mnamo Septemba 22.