• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Wakenya kutisha Dunia riadha za Qatar, AK yasema

Wakenya kutisha Dunia riadha za Qatar, AK yasema

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha watimkaji wa marathon watakaopeperusha bendera ya Kenya katika Riadha za Dunia mwaka huu nchini Qatar kinatarajiwa kuondoka nchini mnamo Jumanne ijayo kuelekea jijini Doha.

Haya ni kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei ambaye ameelezea ukubwa wa matumaini yake kwa kikosi hicho kinachoendelea kujifua mjini Eldoret.

“Hiki kikosi cha marathon ndicho bora zaidi ambacho kitawakilisha Kenya katika historia ya Riadha za Dunia. Nimeridhishwa na kiwango cha maandalizi ya kila mwanariadha na sina shaka kwamba wengi wao watanyakua medali nchini Qatar,” akasema Tuwei ambaye pia alishiriki kikao na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge.

Kipchoge kwa sasa anajiandaa kuwa mwanariadha wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili atakaposhuka jijini Vienna, Austria mwezi ujao kunogesha kivumbi cha “INEOS 1:59 Challenge”.

Ushindi wa Kipchoge katika kivumbi hicho kutamshuhudia akizawidiwa gari aina ya Pick-up lenye thamani ya Sh4.1 milioni kutoka kwa kampuni ya Isuzu.

Kikosi cha wanawake kitakachowakilisha Kenya katika marathon jijini Doha kinawajumuisha bingwa wa Boston Marathon Edna Kiplagat atakayekuwa nahodha, mshindi wa zamani wa Paris Marathon Visiline Jepkesho na malkia wa Dubai Marathon, Ruth Chepng’etich. Geoffrey Kirui, Amos Kipruto na Paul Lonyangata ambaye ni bingwa wa zamani wa Paris Marathon watatoana kijasho kwa upande wa wanaume.

“Tunajikakamua kuhakikisha kwamba vikosi hivi vinashughulikiwa vilivyo wakati vinapojiandaa kuelekea Doha kwa mapambano yatakayong’oa nanga mnamo Septemba 27 kwa upande wa wanawake,” akasema Tuwei kwa kufichua kwamba marathon ya wanaume itafanyika Oktoba 5.

Watimkaji wa Kenya watapania kurejesha kumbukumbu za 2015 ambapo walitawazwa mabingwa wa Riadha za Dunia jijini Beijing, China. AK ilikamilisha shughuli za kuteua timu za fani nyinginezo mnamo Septemba 13 na kwa sasa zinaendelea kujipiga msasa jijini Nairobi zikisubiri kuelekea jijini Doha kwa makundi matatu kati ya Septemba 22- 27.

Wakenya Elijah Manangoi (mita 1,500), Geoffrey Kirui (marathon), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Faith Chepng’etich (mita 1,500) na Hellen Obiri (mita 5,000) watakuwa wakilenga kutetea mataji ambayo walishinda mnamo 2017 Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza.

Kikosi cha Kenya kinanolewa na kocha Julius Kirwa akisaidiana na wakufunzi wengine 10. Mataifa 214 ambayo ni wanachama wa Shirikisho la Raidha Duniani (IAAF) yanatarajiwa kunogesha makala haya ya 17 ya Riadha za Dunia.

Kikosi

Mita 400 Wanaume – Alphas Kishoyian, Emmanuel Korir.

Wanawake – Hellen Syombua, Mary Moraa.

Mita 800 Wanaume – Ng’eno Kipng’etich, Emmanuel Korir, Ferguson Rotich. Wanawake – Eunice Sum, Jackline Wambui.

Mita 1,500 Wanaume – Elijah Manangoi, Timothy Cheruiyot, Ronald Kwemoi, George Manangoi. Wanawake – Faith Chepng’etich, Winnie Chebet.

Mita 3,000 kuruka viunzi na maji Wanaume – Conseslus Kipruto, Leonard Bett, Benjamin Kigen, Abraham Kibiwott.

Wanawake – Beatrice Chepkoech, Hyvin Kiyeng, Celliphine Chespol, Fancy Cherono.

Mita 5,000 Wanaume – Nicholas Kipkorir Kimeli. Wanawake – Hellen Obiri, Lilian Kasait, Margaret Chelimo.

Mita 10,000 Wanaume – Rhonex Kipruto, Rodgers Kwemoi, Alex Oloitiptip.

Wanawake – Agnes Jebet Tirop, Hellen Obiri, Rosemary Wanjiru.

Matembezi ya kilomita 20 Wanaume – Samuel Gathimba . Wanawake – Grace Wanjiru.

You can share this post!

KPL: Bandari na Zoo Kericho kutoana jasho leo Jumatano...

De Gea arefusha mkataba wake Manchester United

adminleo