Michezo

Shikanda asema tiketi za AFC kununuliwa kielektroniki

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa AFC Leopard Dan Shikanda amewahimiza mashabiki wa timu hiyo waendelee kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa kununua tiketi za mechi ili kuzuia msongamano dakika za mwisho kabla mtanange kuanza.

Shikanda alikanusha madai kwamba aliwashutumu mashabiki wa Ingwe kwa kuitoroka timu yao, akisema mashabiki wamekuwa kiungo muhimu na tatizo hasa hutokea wakati wa ununuzi wa tiketi dakika za lala salama kabla ya mechi kuanza.

“Nawadhamini sana mashabiki wa Ingwe kwa kuwa wao ndio injini ya timu hii na wametusaidia sana. Wengine hata hutoa fedha zao binafsi kugharimia safari za timu na hata kujaza magari yetu mafuta. Tatizo hasa limekuwa kuhusu ununuzi wa tiketi kwa njia za kielektronik kwa sababu wengi huzinunua wakiwa wamechelewa na kusababisha msongamano kwenye lango la kuingia uwanjani,” akasema Shikanda kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Afisa huyo wa Ingwe pia aliwaondolea mashabiki hofu kuhusu matatizo ambayo yamekuwa yakikumba mfumo huo mpya, akisema sasa u shwari na kila shabiki wa Ingwe anaweza kununua tiketi na kupata ujumbe haraka iwezekanavyo.

Akanusha

Aidha, alikanusha kwamba aliwachemkia mashabiki kwa kutokuja uwanjani na kuunga timu hiyo na badala yake akasema ufanisi au kuporomoka kwa timu kunawategemea.

“Nilinukuliwa vibaya na ukweli ni kwamba mashabiki wetu hawajatoroka timu. Nawaomba wafike uwanjani kwa wingi na waendelee kuiunga mkono. Nimevamiwa mitandaoni kwamba nipo vitani na mashabiki lakini hilo si kweli kwa sababu AFC Leopards ni timu maarufu, thabiti inayoshabikiwa na wengi,” akaongeza Shikanda.

Wikendi hii Ingwe watakuwa ugenini kwenye patashika kali dhidi ya Wazito FC ugani Bukhungu na Shikanda amewaomba mashabiki kutoka eneo la Magharibi kujaa uwanjani kushushudia mtanange huo.