Okumbi ange kunyakua Cecafa ya makinda U-20
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Stanley Okumbi amekiri kuwa ukubwa wa kiwango cha maandalizi yaliyofanywa na chipukizi wake wa Rising Stars U-20 utawavunia ufalme wa kipute cha Cecafa kitakachoandaliwa nchini Uganda kati ya Septemba 21 na Oktoba 5.
Makinda hao wa Kenya walishiriki kipindi chao cha mwisho cha mazoezi mnamo Jumanne katika Shule ya Kimataifa ya Gems Cambridge, Nairobi.
“Tupo katika kundi gumu. Hata hivyo, naamini kwamba ugumu wa kundi utatuweka katika ulazima wa kujituma maradufu na kukabiliana vilivyo na ushindani mkali,” akatanguliza Okumbi.
“Mbali na ubora wa kikosi cha sasa, kingine kinachotuaminisha zaidi ni hamasa tele inayowatawala wachezaji kambini. Nimewaambia wachezaji wangu kuwa hii ndiyo fursa kwa kila mmoja kudhihirisha uwezo wake uwanjani. Sina shaka kwamba timu itatia fora,” akasema kocha huyo wa zamani wa Mathare United.
Kikosi cha Stars kiliondoka humu nchini hapo jana kuelekea mjini Jinja, Uganda kwa nia ya kunogesha kivumbi hicho kitakacholeta pamoja mataifa 11.
Kenya wametiwa katika Kundi B kwa pamoja na Ethiopia, Zanzibar na Tanzania. Uganda, Sudan, Eritrea na Djibouti wanakamilisha Kundi A huku Kundi C likiwajumuisha Burundi, Sudan Kusini na Somalia.
Vikosi vitavyokamilisha kampeni za Kundi A na B katika nafasi tatu za kwanza vitaungana na wapinzani wawili wengine kutoka Kundi C kwa minajili ya hatua ya robo-fainali.
Wakati uo huo, kocha David Ouma wa Harambee Starlets amefichua kwamba atalazimika kukifanyia kikosi chake mabadiliko makubwa kabla ya kukutana na Ghana katika raundi ya tatu ya mechi za kufuzu kwa Olimpiki za 2020 zitakazoandaliwa jijini Tokyo, Japan.
Black Queens ya Ghana ilifuzu kuchuana na Kenya baada ya kupepeta Gabon 2-0 katika mkondo wa pili, na hivyo kusajili ushindi wa jumla ya mabao 5-0 uliowapa tiketi ya kuchuana na Starlets waliobandua She-Flames ya Malawi.
Safu ya Ulinzi
Ingawa hivyo, Ouma amekiri kwamba kinachomkosesha usingizi ni udhaifu wa kikosi chake katika safu ya ulinzi, jambo ambalo litamweka katika ulazima wa kuisuka upya timu hiyo kabla ya kushuka dimbani kupimana ubabe na Ghana. Mchuano wa mkondo wa kwanza kati ya Ghana na Kenya utasakatwa Septemba 30 jijini Accra kabla ya marudiano kuandaliwa Nairobi mnamo Oktoba 4. Itakuwa ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana.
Mnamo 2017, Ghana waliwapepeta Starlets 3-1 katika mojawapo ya mechi za fainali za Kombe la Afrika (AWCON) kisha kuambulia sare walipokutana kirafiki jijini Nairobi mwaka uliopita.
Chini ya Ouma, Starlets waliwapepeta Malawi 3-0 waliporudiana ugani Kenyatta, Machakos baada ya chombo chao kuzamishwa kwa 3-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliotandazwa jijini Blantyre.
Katika mechi ya mkondo wa pili ambayo Kenya ilicheza bila mashabiki kwa sababu Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) halijaidhinisha uwanja wa Machakos kuandaa mechi za kimataifa, Starlets walihitaji ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele.