• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
MAARIFA YA UFUGAJI: Alibadili mfumo wa ufugaji, maziwa yakajaa mara 13!

MAARIFA YA UFUGAJI: Alibadili mfumo wa ufugaji, maziwa yakajaa mara 13!

Na PETER CHANGTOEK

LICHA ya kuzipitia changamoto awali katika shughuli ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, Nyaga Muchina hakufa moyo abadan kataan, bali aliubadilisha mtindo aliokuwa akiutumia katika kilimo hicho, na kwa wakati huu anayazalisha maziwa takriban lita 550 kwa siku moja, badala ya lita 40 alizokuwa akipata.

Muchina, 36, alijitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mnamo 2002, katika kitongoji cha Mwireri, Ol Kalou, Kaunti ya Nandarua, pindi tu alipokamilisha masomo yake ya shule ya upili. Baada ya kuiona shauku ambayo mwanawe alikuwa nayo kwa masuala ya kilimo, baba yake alimkabidhi ng’ombe wawili.

Kwa sasa, analitumia shamba la ekari ishirini kuiendesha shughuli hiyo, na ng’ombe wake hutandikiwa matandiko maalumu, huku wakiongolewaongolewa kwa miziki ya kuvutia. Aidha, hupewa lishe aula ili wayazalishe maziwa kwa wingi.

Ng’ombe wake wawili waliongezeka kadiri miaka ilivyosonga, hadi wakafikia saba kwa idadi. Hata hivyo, alipitia changamoto kadhaa k.v kutoyapata maziwa mengi licha ya kuwalisha ng’ombe wake kwa lishe nyingi. Alikuwa akiyazalisha maziwa yasiyopita lita 40 kutoka kwao.

Mnamo mwaka 2012, mkulima huyo, pamoja na wenzake walilizuru shamba moja lililokuwa katika kaunti ya Kiambu. Ziara hiyo iliandaliwa na shirika la Ol Kalou Dairy, lililokuwa likiyanunua maziwa kutoka kwa wakulima hao.

Miongoni mwa mambo ambayo wakulima hao walifunzwa katika ziara hiyo ni kuwa wangeweza kuyazalisha maziwa zaidi ya lita 40 kutoka kwa ng’ombe mmoja aina ya Friesian, muradi tu alishwe ipasavyo.

Baada ya kuyapata mafunzo hayo, akaamua kuwauza ng’ombe wake wote saba na kumnunua mmoja mwenye uwezo wa kuyazalisha maziwa lita 35 kwa siku. Hata hivyo, ng’ombe huyo akayazalisha maziwa lita 40 kwa sababu ya kulishwa vyema.

Alipata hamu na ghamu ya kuwa na ng’ombe zaidi ya mmoja alipoona kuwa huyo alikuwa akiyazalisha maziwa mengi na akaamua kuwanunua wengine wawili, na maziwa aliyokuwa akiyapata yakaongezeka hadi zaidi ya lita 100 kwa siku.

Mkulima huyo, kwa wakati huu anafahamu fika kwamba kuwalisha ng’ombe kwa lishe bora humwezesha mkulima yeyote kuyapata maziwa mengi. Yeye huwalisha ng’ombe wake mara mbili kwa siku.

Anasema kuwa ng’ombe hawafai kulishwa kwa lishe za kijani zenye unyevu mwingi. Kwa hivyo, yeye huhakikisha kuwa wanalishwa kwa lishe zilizokauka zenye protini, kabohaidreti na madini mengine.

“Lishe zisizokuwa na unyevu huwafanya ng’ombe kuyanywa maji mengi na hivyo kuzalisha maziwa mengi,’’ asema Muchina, ambaye alisomea taaluma ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

Katika juhudi zake kuhakikisha kuwa kuna lishe za kutosha kuwalisha ng’ombe wake kila wakati, mkulima huyo aliipanda mimea ambayo hutumiwa kuzitengeneza lishe. Muchina pia huzinunua lishe za mifugo zinazouzwa madukani ili kuchanganya nazo.

Ng’ombe hao hukamwa mara tatu kwa siku, ambapo yeye hupata maziwa takriban lita 550 kwa siku kutoka kwa ng’ombe kumi wenye uwezo wa kutoa maziwa mengi. Kwa mwezi mmoja, mkulima hupata takriban Sh350,000 baada ya kuondoa gharamu ya uzalishaji.

 

Nyaga Muchina aonyesha matandiko ya ng’ombe wake. Picha/ Peter Changtoek

Wakulima wengi hulizuru shamba lake ili kupata mafunzo kuhusu jinsi ya kuyazalisha maziwa mengi. Wao hulipa Sh250 ili kupata mafunzo kuhusu uzalishaji wa maziwa.

Yeye huwatandikia ng’ombe wake matandiko maalumu.

“Ng’ombe anayelala sakafuni hawezi kuyazalisha maziwa yanayotakikana,’’ Muchina afichua.

Mkulima huyo huwalisha kwa lishe kilo 15 asubuhi na kilo 15 jioni. Anatahadharisha kuwa ng’ombe hawafai kulishwa kwa lishe zinazokithiri kiasi kinachofaa.

Muchina, ambaye ana wafanyakazi watano, huzitumia mbolea kutoka kwa mifugo yake kuikuza mimea shambani na hivyo kuipunguza gharama ya uzalishaji wa mazao.

Anawashauri wale wanaoazimia kujitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kuhakikisha kwamba wana lishe zinazotosha kuwalisha ng’ombe kwa mwaka mzima, kabla hawajajitosa katika shughuli hiyo.

Mkulima huyo ameungana na wenzake ili kuboresha thamani ya maziwa. Amezinunua mashine kutoka ughaibuni zinazotumika kwa shughuli hiyo. Mashine hizo zinaweza kutengeneza na kupakia maziwa lita 3,500 kwa siku moja.

Mbali na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, mkulima huyo, pia, huwafuga nguruwe na kuku.

Anawasihi vijana kujitosa katika kilimo biashara, badala ya kujichosha wakitafuta ajira ambazo aghalabu ni nadra kuzipata.

 

  • Tags

You can share this post!

Nema yavitaka vituo vya afya kufuata utaratibu muhimu...

Mtoto mchanga apatikana katupwa kando ya lori mjini Thika

adminleo