Soka inavyotumiwa kuzima uhalifu
Na SAMMY WAWERU
Awali mtaa wa Githurai, Nairobi ulikuwa wenye sifa kuntu za uhalifu lakini sasa taarifa za aina hiyo zinapungua.
Ni visa vichache vya mitandao ya magenge ya uhalifu vinavyoripotiwa, hasa kwa waliotia maskio yao nta.
Hii ni kutokana na kuimarishwa kwa usalama kupitia ushirikiano wa karibu wa maafisa wa polisi, wanakijiji na wadau husika.
Mbali na idara ya usalama kushika doria, baadhi ya miungano na makundi ya kijamii yamejituma kunasua vijana waliotekwa na minyororo ya uhalifu.
Aidha, washirika hao wanatumia sanaa kama vile michezo ya kuigiza, filamu na mashairi, ambapo kando na kuangazia uhalifu, pia wanahamasisha kuhusu magonjwa hatari ya zanaa kama Ukimwi.
Michezo kama vile soka na voliboli pia inatumiwa kuwaokoa, ambapo ukizuru mtaa huo na viunga vyake kila siku majira ya jioni na wikendi utawaona vijana wakishiriki. Ni hamasa ambayo kwa hakika imekuwa afueni kwa vijana, wengi wakiitumia kama jukwaa kutambua vipaji vyao, wanavipalilia na kuvitumia kama kitega uchumi.
Historia ya mtaa huo ikinakiliwa, jina la Fredrick Ochieng halitakosa kujumuishwa. Bw Ochieng ni mwasisi na mwanzilishi wa timu ya Githurai United ambayo pia imezaa All Stars Githurai.
Ni timu ambayo imebatiza na kuokoa vijana wengi waliodhani njia pekee kuzimbua riziki ni kushiriki uhalifu.
Mwasisi Ochieng ambaye pia ni kocha, alianzisha harakati hizo 1998. “Ni baada ya kuona vijana wakipoteza maisha kupitia uhalifu. Githurai United pia baadaye ilipata tawi la All Stars Githurai, ni kama kituo cha kurekebisha tabia na maadili, na kupitia wazo hilo wengi wamekuwa mastaa katika kabumbu,” afafanua.
Kushirikisha vijana katika kandanda, Bw Ochieng anasema kumesaidia kuleta taswira mpya Githurai, mtaa ambao kwa sasa unafanya biashara usiku na mchana. “Baadhi ya wafanyabiashara wanaendesha gange zao usiku na mchana, suala ambalo lilikuwa tete hapo awali kwa sababu ya mmomonyoko wa hali ya usalama,” asema.
Kitambo ilikuwa vigumu kwa yeyote kuwekeza biashara eneo hilo kwa kile kilitajwa kama ‘mtaa hatari, potovu na uga wa wizi’. “Duka langu linahudumu saa 24 ishara kuwa usalama ni shwari,” aungama Antony Kibui, mfanyabiashara.
Kukuza vipaji tajika
Mbali na wazo la Bw Ochieng kuangazia pakubwa usalama, limekuwa kinoleo cha vipaji ambapo kadhaa wameibuka kuchezea vilabu tajika vya soka nchini na rubaa za kimataifa. Francis Kahata ambaye amekuwa kiungo wa kati na mshambuliaji hodari wa Gor Mahia FC, kilabu inayocheza ligi za kitaifa Kenya, KPL, alichomolewa Githurai United.
Bw Kahata kwa sasa anachezea klabu ya Simba SC iliyoko nchini Tanzania kama kiungo wa kushoto au kiungo mshambuliaji, na Ochieng anasema alipitia mikononi mwake.
Wengine ambao timu ya Githurai United inajivunia kunoa ni Peter Nzuki wa Tusker FC, Kevin Kimani na David Okello wa Mathare United. Pia, Danson Kago, Kevin Odongo na Samuel Mbugua, watatu hao wakisakatia ngozi Posta Rangers, wamepitia mikononi mwa Ochieng, listi hiyo ikiwa chache tu kuiorodhesha.
“Ni fahari kuu kuona vipaji niliowachukua wakiwa wachanga na kuwanoa kufikia kiasi cha kuwakilisha nembo ya Githurai United katika vilabu tajika nchini, hususan zinazoshiriki michuano ya KPL,” anasema kocha huyo, akiongeza kusema kuwa Githurai United inajumuisha vipaji wa Githurai na mitaa jirani.
Anaendelea kueleza kwamba baadhi ya mastaa wamesajiliwa kujiunga na vikosi vya polisi nchini (NPS) na wanajeshi (KDF) ili kuviwakilisha katika soka.
Mwenyekiti wa Githurai United Charles Njenga anasema wana kila sababu ya kutabasamu kuona mtaa ulioaminika kupotoka kimaadili ukiwa na mastaa wanaowakilisha vilabu maarufu vya soka nchini. “Mbali na kuangazia suala la uhalifu, utumizi wa mihadarati na dawa za kulevya na pombe, tumenoa talanta za wanasoka wanaosakatia ngozi vilabu tajiaka nchini,” aeleza, akiongeza kuwa mastaa wengi wamepata ajira.
Viunzi wanavyoruka
Uga wanaotumia kunoa vipaji chipukizi u pembezoni mwa shule ya msingi ya Githurai, Nairobi. Aidha, huendesha shughuli hiyo majira ya jioni, wikendi na wakati wa likizo.
Kwa kuwa hakuna chema kisichokosa doa, Kocha Ochieng anasema ukosefu wa ufadhili ndicho kizingiti kikuu cha Githurai United kuimarika. Ukosefu wa vifaa maalumu kama majezi, viatu na hata nauli kusafiri kushiriki mechi inawatatiza.
“Ili kushiriki mechi hulazimika kukodi uga kwa ada kati ya Sh3,500 – 20, 000 kila mchuano. Nauli ya kusafiri wakati wa mechi pia ni balaa. Tunapata usaidizi kifedha kutoka kwa mashibiki na wasamaria wema,” aeleza.
Isitoshe, uwanja inaotumia kufanya mazoezi umesheheni vumbi, hali hiyo ikiwatia katika hatari ya kuugua magonjwa yanayosababishwa na vumbi.
Juhudi za timu hiyo kuomba ufadhili kwa viongozi waliochaguliwa kama vile madiwani na mjumbe wa eneobunge la Mwiki, zimegonga mwamba. “Majibu tunayopata ni ya kufisha ari zetu, tena suala la kupigwa jeki limegubikwa na siasa duni zingine zikiwa za kikabila, hivyo basi inakuwa vigumu kufuatilia ufadhili,” akalalamika Bw Ochieng wakati wa mahojiano.
Kocha huyo alisema timu yake ingekuwa na uwezo kifedha, ingekuwa ikilipa wachezaji wake ili kuwapa motisha.
Makadirio ya bajeti ya kila mwaka, hazina ya kitaifa hutengea idara ya michezo fedha za kuistawisha, pamoja na kupalilia vipaji chipukizi nchini. Ni mgao usiofikia timu hiyo na zinginezo nchini.
Ili kupalilia vipaji chipukizi, Ochieng amegawanya mazoezi kwa makundi matano; walio chini ya umri wa miaka 10, 12, 14, 16 na zaidi ya 18.
Walio zaidi ya miaka 18, ndio hupeperusha bendera ya Githurai United katika michuano mbalimbali. Timu hiyo imeshiriki michuano ya ligi ya FKF, Super 8 na tonamenti ya Koth Biro.