• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
KCB na PFC zakubaliana kukuza vipaji

KCB na PFC zakubaliana kukuza vipaji

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya KCB FC imeingia mkataba wa muda mrefu na Protege Football Club (PFC) kwenye jitihada za kukuza wachezaji chipukizi na kuwapa nafasi kuichezea KCB FC katika Ligi Kuu ya KPL miaka ijayo.

Timu hizo zilifikia hatua hiyo baada ya kukamilika kwa mechi za majaribio ambapo PFC ilinasa vijana 36 miongoni mwa wachezaji 100 walioshiriki zoezi hilo.

”Chipukizi hao watajiunga na wenzao katika familia ya PFC ambapo kando na kupata nafasi ya kuchezea vikosi vya juu pia watapata mwanya mzuri kupalilia talanta zao katika mchezo huu,” alisema ofisa mkuu wa PFC, Steve Othoro na kuongeza kuwa kupitia ushirikiano huo wanatarajia kupiga hatua katika makuzi wa mchezo huo nchini.

Alidokeza kuwa tangia mwaka 2008 jumla ya wachezaji 80 wamefaulu kupitia kituo hicho na kuzipigia vikosi mbali mbali pia kushiriki soka la kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya.

”Bila shaka tuna furaha tele kufanya kazi na PFC ambayo imeonyesha imejiweka vizuri kukuza talanta za chipukizi wanaokuja,” alisema meneja wa KCB, Bramwel Mbirira na kuongeza kuwa wanatarajia mafanikio zaidi hasa kwenye juhudi za kujaza nafasi katika kikosi cha KCB FC cha wakubwa kinaoshiriki Ligi Kuu ya KPL.

Hatua hiyo inaenda sambamba na mwito wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ambalo linalozitaka klabu zote zinazoshiriki Ligi ya KPL pia kuwa na timu ya wachezaji chipukizi.

PFC pia ina kikosi cha wasiozidi umri wa miaka 19 ambacho hushiriki kipute cha Ligi ya Kaunti ya Nairobi. Kadhalika inajivunia wachezaji wawili, Eric Kinuthia na Ronald Bebeto walioteuliwa katika kikosi cha taifa cha U-20 kilichosafiri nchini Uganda kushiriki mechi za ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Vikosi vya KPL ambavyo pia vina timu za chipukizi ni pamoja na Gor Mahia FC, AFC Leopards, Zoo Kericho, Sony Sugar na Tusker FC kati ya zingine.

You can share this post!

Kinyago na Volcano vitani ligi ya KYSD

‘Wanaopigwa msasa kuongoza NLC ni wafisadi’

adminleo