• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Watimkaji 14 barani ange kushiriki mbio za Safaricom Mombasa

Watimkaji 14 barani ange kushiriki mbio za Safaricom Mombasa

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WANARIADHA 14 kutoka mataifa ya Afrika wamethibitisha kushiriki kwao kwenye Mbio za Kimataifa za Safaricom Mombasa za Kilomita 10 zitakazoanza na kumalizikia Treasury Square siku ya Jumapili.

Mwenyekiti wa Chama cha Riadha nchini (AK) tawi la Mkoa wa Pwani, Dammy Kisalu amesema mshindi wa Mbio za mwaka 2017 za Philadelphia Half Marathon, Panuel Mkungo anatarajia kuongoza washindani wa Kenya dhidi ya wakimbiaji kutoka nchi nyingine za Afrika.

Hadi Alhamisi asubuhi, wakimbiaji wa nje ya Kenya waliothibitisha kushiriki mbio hizo ni mshiriki mmoja mmoja kutoka mataifa ya Ethiopia, Eritrea, Djibouti na Zanzibar kisha pia kuna wakimbiaji wawili kutoka Rwanda na watano kutoka Tanzania wamethibitisha kushiriki.

“Wanariadha hao ndio waliothibitisha kwetu kuwa watakuwako kupigania ushindi kwenye mbio hizo ambazo tunazitayarisha kwa mara ya kwanza na tutazifanya kuwa za kila mwaka,” akasema Kisalu ambaye alieleza matumaini yao kuwa wakimbiaji wenye majina makubwa nchini watashirikii.

Aliambia Taifa Leo kuwa mbio hizo za Jumapili zitakuwa za kuziondoa mbio zilizokuwa zikifanyika kila mwaka za Mombasa International Marathon ambazo sasa hazitafanyika tena kutokana na wadhamini wake wa Safaricom kupunguza fedha za udhamini wake.

“Wadhamini wetu wa Safaricom wamepunguza udhamini wao kutoka Sh2 milioni hadi Sh1 milioni na hivyo kutotosha kuandaa mbio za marathon na ndio maana badala yake tumeanzisha mbio za kilomita 10 za kimataifa,” akasema Kisalu.

Sheria za AK zinataka washindi wa marathon watunukiwe kiwango cha zawadi kisichopungua Sh500,000.

“Udhamini wa Sh1 milioni ni mdogo sana kwa tawi letu kutayarisha mbio za marathon na hivyo tumeonekleqa tuanzishe mbio mpya za kilomita 10,” akasema.

Zawadi

Kinara huyo wa AK Pwani alitangaza kuwa washindi wa mbio hizo za kilomita 10 kwa wanaume na wanawake watatuzwa kitita cha Sh100,000 kila mmoja na washindi wa pili na watatu kuondoka na zawadi za pesa taslimu Sh50,000 na Sh30,000 mtawalia.

Washindi wa nne watapata Sh20,000 watano Sh10,000 hali wa sita hadi wa kumi kupata Sh5,000 kila mmoja.

Kulingana na Kisalu, kutakuwa na zawadi za pesa kwa washindi kumi wa Mkoa wa Pwani watakaomaliza mbio hizo ambapo washindi wa vitengo vya wanaume na wanawake kila mmoja atapata Sh20,000, wapili kutia kibindoni Sh15,000, watatu Sh10,000, wanne Sh5,000, watano Sh4,000 na wa sita Sh3,000.

Washindi was aba hadi wa kumi kila mmoja ataondoka na Sh2,000.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Katika maisha ya leo yatubidi tuwe na...

Kenya yatuama katika nafasi ya 107 Fifa

adminleo