Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mtetezi halisi wa wanawake na watoto

September 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na KEYB

KWA miaka, amekuwa sauti kuu katika vita dhidi ya ubakaji, dhuluma za kimapenzi na utetezi wa haki za wanawake na watoto nchini Kenya.

Kutana na Fatma Abeyd, mwanzislishi wa Kenya Anti-Rape Organization (KARO), shirika ambalo dhamira yake ni kupambana na ubakaji na dhuluma zingine za kimapenzi.

Mbali na hayo Bi Abeyd pia amehusika katika kampeni mbalimbali za kutetea maslahi ya wanawake na wasichana, vile vile uhifadhi wa mazingira miongoni mwa mambo mengine katika jamii.

Na kutokana na jitihada zake za kuwahudumia watoto na wanawake, ametunukiwa tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ford Foundation Award, the Peace Foundation of Africa Award: Human Rights, na Guinness Stout Effort Award of 1993.

Aidha, mwaka wa 1994, alitwaa tuzo ya Tangaza College of Theology of the Catholic University of East Africa kutokana na vita vyake kupigania haki za wanawake na watoto.

Mwaka wa 2006, mashirika ya Coalition on Violence Against Women (COVAW), na International Rescue Committee yalimtangaza kama bingwa katika jitihada za kuzuia na kukabiliana vilivyo na dhuluma.

Mwaka wa 2009 katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuwatambua wanawake, alipokea tuzo ya Unsung Hero Award huku Balozi wa Amerika nchini wakati huo, Michael Ranneberger, akisema kwamba hii ilikuwa ni kutokana na jitihada zake kuwapa wanawake na wasichana sauti.

Pia, juhudi zake za kutetea maslahi ya wasichana na wanawake zimemfanya kusafiri mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Austria, Uholanzi na China, miongoni mwa mengine.

Bi Abeyd alizaliwa mwaka wa 1947, ambapo alijiunga na shule ya msingi ya Kibera na baadaye kusomea katika shule ya upili ya Nairobi Girls School (ambayo kwa sasa inafahamika kama Moi Girls’ School Nairobi). Mwanzoni alifanya kazi kama mtangazaji katika idhaa ya Kiswahili ya kituo cha Sauti ya Kenya (VoK), na baadaye kuhudumu katika hoteli za InterContinental na Serena, kabla ya kufanya kazi kama mhudumu wa kujitolea katika mashirika ya Green Belt Movement na Kibera Campaign against Dumping.

Mzaliwa wa kitongoji duni maarufu cha Kibera, ari yake ya kutaka kuleta mabadiliko katika maisha ya wanawake na wasichana ilianza akiwa na miaka kumi pekee.

“Nilishuhudia mamangu akijifungua kwa usaidizi wa wakunga wa kiasili, na kutokana na kutokuwepo na huduma za kimatibabu, watoto hao walifariki. Niliwasikia wakunga wakisema kwamba watoto hao hawakuwa wamefikisha siku za kuzaliwa na kwamba hawangeweza kuwaokoa,” aeleza.

Baadaye Bi Abeyd alishuhudia visa kadha wa kadha vya ukiukaji wa haki za kibinadamu, kama vile ubomoaji uliotekelezwa katika miaka ya tisini mtaani Kibera.

Mwaka wa 1991, alizindua shirika la kupigana dhidi ya ubakaji la KARO, ambalo kubuniwa kwake kuliibua hisia kali hasa kutokana na masuala ambayo lilinuia kuangazia.

Shirika hili lilisajiliwa wakati ambapo mkasa wa ubakaji wa Julai 13, 1991 katika shule mseto ya upili ya St Kizito, Meru ulikuwa umewaacha wengi vinywa wazi. Katika kisa hicho, wasichana 19 walifariki huku wengine 72 wakijeruiwa.

“Tukio hili lilifungua macho ya jamii kwamba masuala ya ubakaji yalipaswa kuzungumziwa hadharani,” asema.

Tukio sawa na hilo lilifanyika mwaka wa 1993, ambapo Mkenya wa asili ya kihindi aliachiliwa huru baada ya kuwabaka wasichana watano.

“KARO iliandaa maandamano ya amani jijini Nairobi. Nilitiwa nguvuni, kudhulumiwa na kushtakiwa mahakamani. Profesa Maria Nzomo alinisaidia kwa kuleta pamoja mashirika ya wanawake na mawakili kuunga mkono kesi hii,” akumbuka.

Vita vyake kutetea haki za kibinadamu vilianza hata kabla ya kuzindua shirika la KARO.

Kama Mnubi katika kitongoji duni cha Kibera, alishuhudia uhasama dhidi ya jamii yake; matukio ambayo mara nyingi hayakuripotiwa.

“Kuna nyakati ambapo kitongoji duni hiki kiligeuzwa na kuwa jaa la taka la viwanda na hospitali. Kuna wakati ambapo hata ungekumbana na vijusi, sehemu za miili na vifaa vingine hatari,” aeleza.

Aliripoti visa hivi kwa Mkuu wa Wilaya, aliyemshauri kuwasilisha malalamishi yake kwa maandishi. “Kisha siku moja ilitangazwa redioni kwamba yeyote atakayepatikana akitupa taka atakamatwa,” asema. Hii ilimpa ari ya kutaka kuleta mabadiliko zaidi katika jamii.

Aidha vita vyake dhidi ya ubakaji vilichochewa zaidi alipokuwa akifanya kazi kama karani katika Shirikisho la wanawake mawakili nchini (FIDA).

“Baada ya kuingiliana na mawakili nilianza kuelewa kuhusu masuala niliyohisi kwamba hayakuwa yakishughulikiwa vilivyo,” akumbuka.

Shughuli hizi zilimsukuma kwenye siasa ambapo jaribio lake la kuwania kiti cha ubunge cha eneo la Lang’ata mwaka wa 1997, liligonga mwamba.

Lakini ushawishi wake ulikuwa tayari unahisiwa kwani mwaka huo huo alichaguliwa kama naibu mwenyekiti wa Kenya Social Congress-KSC.

Kampeni siku 16

Mwaka wa 1993, aliongoza kampeni za siku 16 dhidi ya dhuluma za kijinsia nchini. Siku hizi 16 zilifikia upeo Desemba 10, tarehe rasmi ya kuadhimisha siku ya haki za kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Aidha, mwaka wa 2002, aliwakilisha maeneo bunge ya Lang’ata na Dagoretti katika tume ya kurekebisha katiba ya Kenya.

Anatambua shirika la KARO kwa kuchangia kupitishwa kwa Sheria Dhidi ya Dhuluma za kimapenzi 2006. Vile vile anasema kwamba shirika hili lilitoa jukwaa kwa mashirika mengine yanayokabiliana na dhuluma za kijinsia.

Kwa sasa Bi Abeyd anazidi kujihusisha na mipango ya maslahi ya kijamii.

Anasimamia kituo cha Stawi Junior Child Centre kinachowashughulikia watoto chini ya miaka minane waliowahi kupitia ukatili huu au wanaoajiriwa licha ya umri wao mdogo.

Pia, anasimamia Kenya Grassroots Leaders Network mtaani Kibera, mradi unaohusika na shughuli za kunasihi vijana na kuhamasisha watu kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Anatoa changamoto kwa serikali kumakinika na masuala ya ubakaji jinsi ilivyochangamkia masuala ya ukeketaji. Anapendekeza kuwepo na mahakama ya papo hapo ili kusaidia kesi za ubakaji kushughulikiwa upesi.