Michezo

Miruara na Kimeli washinda mbio za Safaricom Mombasa

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WATIMKAJI Delvin Miruara na Mathew Kimeli wametia kibindoni Sh100, 000 kila mmoja baada ya kunyakua mataji ya mbio za kilomita 10 za Mombasa, Jumapili.

Katika mbio hizi zinazodhaminiwa na kampuni ya Safaricom, Miruara alikata utepe kwa dakika 36:10.45. Nafasi ya pili ilinyakuliwa na Cynthia Kosgei (37:00.36) naye Roseline Chepketer akaridhika katika nafasi ya tatu (37:22.95).

Kimeli, ambaye mwezi Agosti alitwaa taji la mbio za kilomita 10 za Iten katika kaunti ya Elgeyo-Marakwet, alitumia dakika 31:27.23 kuibuka mshindi.

Alifuatwa kwa karibu na Stephen Mwendwa (31:38.76) na Solomon Kiplimo (31:45.23), mtawalia.

Nambari mbili na tatu katika vitengo vyote viwili walitunukiwa Sh50,000 na Sh30,000, mtawalia.

Baada ya ushindi, Miruara alisema, “Hali ya anga ilikuwa mbaya, lakini mazoezi mazuri yalinisaidia kuibuka na ushindi huu. Najiandaa kuelekea katika kaunti ya Taita Taveta kushiriki mbio za kilomita 21 za Madoka Half Marathon.”

Mbio zilizosalia katika ratiba ya Safaricom ya mwaka 2019 ni Madoka Half Marathon mnamo Oktoba 5, mbio za nyika za Isaiah Kiplagat Memorial Ndalat na mbio za barabarani za Mombasa, Kisii, Imenti na Kisumu.

Matokeo (tano-bora):

Wanaume

Mathew Kimeli saa 32: 27.23

Stephen Mwendwa 31:38.76

Solomon Kiplimo 31:45.23

Bernard Musa 31:55.16

Panuel Mkungo 32:06.95

Wanawake

Delvine Meringor dakika 36:10.45

Cynthia Kosgei 37:00.36

Roseline Chepketer 37:22.95

Naomi Kemunto 38:02.20

Christine Ndanu 38:21.04