• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
SHANGAZI AKUJIBU: Ninahisi kijana ameniharibia miaka mitatu bure

SHANGAZI AKUJIBU: Ninahisi kijana ameniharibia miaka mitatu bure

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 21 na nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana fulani kwa miaka mitatu. Nimefikiria kwa makini kuhusu uhusiano wetu na muda ambao tumekuwa pamoja na kuhisi kuwa nimepoteza wakati wangu kwa sababu sijaona lolote la maana kwake hata hisia zimetoweka. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kwa kifupi, ina maana kwamba umegundua kuwa humpendi kijana huyo na hutaki kuendelea na uhusiano huo. Kama ndivyo, ni muhimu umwelezee ukweli huo mapema ili muachane, kila mmoja wenu aendelee na maisha yake. Uliingia katika uhusiano huo kwa hiari na una haki ya kujiondoa.

 

Mke wangu haachi kuvuta sigara licha ya kutoa ahadi na kupata mtoto wa pili, nifanyeje sasa?

Kwako shangazi. Nilimuoa mke wangu akiwa na mtoto mmoja wa kike. Huu ni mwaka wa pili tangu tuoane na tumepata mtoto mwingine wa kiume. Tulipokutana alikuwa anavuta sigara na akaniahidi kuwa ataacha kwa sababu mimi sivuti sigara wala sipendi harufu yake. Lakini ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo na mpaka wa leo hajaacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tunaambiwa kuwa ahadi ni deni. Kama mojawapo ya maafikiano kati yenu kabla ya ndoa ilikuwa ni mke wako kuacha kuvuta sigara; na aliahidi kufanya hivyo, ni muhimu atimize ahadi yake hiyo. Kwake kukosa kutimiza ahadi yake ni kuhatarisha ndoa yenu kwani unasema huwezi kuvumilia harufu ya sigara. Mwambie wazi ili aamue kati ya ndoa na uraibu wake huo.

 

Mpenzi amekataa nikionja tunda miaka kadhaa tangu tuwe pamoja, nashuku ananiharibia wakati?

Hujambo shangazi? Nina mpenzi ambaye tumekuwa na uhusiano kwa muda mrefu sana. Ajabu ni kwamba amekataa kabisa kunionjesha asali licha ya kudai kwamba ananipenda. Je, ninapoteza wakati wangu?

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati yanatoka moyoni mwa mtu na si lazima mtu akubali kushiriki tendo la ndoa ili kuyathibitisha. Wapo watu wengi wanaoshiriki tendo hilo bila mapenzi. Pili, kitendo hicho ni halali tu kwa watu walio katika ndoa. Kama mwenzako amekuhakikishia kuwa anakupenda, huna sababu ya kumshuku. Subiri hadi utakapomuoa ndipo akupe haki yako.

 

Mke wangu anikataza haki yangu chumbani na tulioana majuzi tu, nipe ushauri

Hujambo shangazi? Nina jambo ambalo linahitaji ushauri wako. Nilioa hivi majuzi tu lakini mke wangu ananitesa. Kisa ni kwamba ananinyima haki yangu ya chumbani bila sababu ya maana. Nikimwambia namhitaji, anasema hajisikii ilhali ni mke wangu ambaye nimemlipia mahari. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Tabia ya mke wako ni kinyume sana na maadili ya ndoa. Huduma za chumbani ni haki na wajibu mkubwa wa mke kwa mumewe na mume kwa mkewe. Hii ndiyo njia pekee ya kupata watoto na kujenga familia. Yamkini mke wako ana sababu kubwa ya kususia wajibu huo na ambayo hataki kukuelezea. Labda amegundua kuwa alikosea kuolewa na wewe. Ushauri wangu ni kwamba uwahusishe wazee kutoka pande zote mbili wamhoji ili wajue kiini hasa cha tabia yake hiyo na suluhu yake.

 

Nashindwa kuambia mwanamke kuwa ninampenda sababu naogopa atanikataa, nishauri tafadhali

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamke ambaye amenivutia kimahaba naye pia naamini ananipenda. Lakini nimekawia kumwambia kwa hofu kwamba atanikataa. Naomba ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Mapenzi yanatokana na wawili kupendana. Unapoamua kumdokezea mtu hisia zako za kimapenzi kwake, unafaa kujua kuwa anaweza kukubali ama kukataa. Unaweza kukataliwa na wanawake kadhaa kabla umpate anayekupenda. Iwapo unatarajia kupata mpenzi, ni lazima pia uwe tayari kukataliwa. Mwelezee hisia zako mwanamke huyo. Kama anakupenda atakwambia, kama hakutaki pia atakwambia.

You can share this post!

KWA KIFUPI: Sababu za mvi kuota mapema

KK Homeboyz yapiku Gor, Bandari katika ngazi ya ligi

adminleo