Makala

MAPITIO YA TUNGO: Mfano Mwema ni hadithi inayowawekea watoto msingi imara wa uadilifu

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Jina la utungo: Mfano Mwema

Mwandishi: Eunice W. Ng’ang’a

Mchapishaji: Oxford

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kitabu: Hadithi ya watoto

Kurasa: 26

‘MFANO Mwema’ ni kisa ambacho kinasimuliwa kupitia kwa babu.

Ni hadithi yenye uhalisia ambayo imedhamiriwa kupitisha funzo la uadilifu kwa watoto.

Babu anakisimulia kisa cha Zakayo ambaye akiwa njiani na wenzake kwenda shuleni anakiokota kibeti chenye bunda la noti.

Baadhi ya wanafunzi wanamshauri kukipeleka kibeti chenyewe kwa mwalimu mkuu ili asaidie katika kumtafuta mwenyewe. Hata hivyo, wapo wanafunzi wengine wanaoiona ile kuwa bahati njema. Wanamshawishi Zakayo wagawane zile pesa kisha wakitupe kibeti chenyewe.

Katikati ya vishawishi hivi, Zakayo anasawiriwa kuwa kijana mwenye msimamo usiotetereka.

Anawaeleza wenzake kwamba ni lazima wakipeleke kibeti chenyewe kwa mwalimu mkuu. Wanafunzi wanaotaka wagawane pesa wanatishia kumpiga Zakayo na kumnyanganya kibeti chenyewe. Zakayo anatimua mbio hadi kwenye ofisi ya mwalimu mkuu na kumkabidhi kibeti kile.

Mwalimu mkuu anapoliona bunda la noti kwenye kibeti, anamgeukia Zakayo na kutamka maneno ya kumpongeza, “Wewe ni kijana mwema. Wewe ni mtoto mwaminifu…’’

Mwalimu mkuu ambaye anavutiwa na tabia ya Zakayo anamshika mkono na kuandamana naye hadi kwenye chumba cha walimu na kumtangaza mbele yao. Kileleni mwa hadithi, inafichuka kwamba kibeti ambacho Zakayo alikiokota kilikuwa cha mwalimu mgeni ambaye alikuwa amehamishiwa shuleni kwao.

Uaminifu na kuwa na msimamo usiotetereka ni tabia ambazo zinapaswa kufunzwa watoto mapema maishani. ‘Mfano Mwema’ ni miongoni mwa kazi bora za kubuni ambazo lengo lake ni kupitisha maadili ya aina hiyo kwa wanafunzi.

Mwandishi wa kazi yenyewe ametumia lugha sahili ambayo inaeleweka kwa wanafunzi wa darasa la nne. Ni kazi ambayo watoto wa kiwango hiki cha elimu wanaweza kuisoma kwa kikao kimoja kutokana na urefu wake usiochosha.

Michoro kitabuni pia inaifanya kazi yenyewe iwe faafu kwa watoto. Ni michoro ya rangi inayokwenda sambamba na masimulizi. Aidha, ni michoro ya rangi inayokumbatia uhalisia.

Mhusika mkuu ambaye ni Zakayo anajitokeza kwingi katika kazi hii jambo linalolifanya rika lengwa kujinasibisha naye kwa urahisi.